1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Tunatarajia bidhaa zitaanza kupita Bahari Nyeusi

14 Julai 2022

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema alikuwa na imani wapatanishi katika vita vya Urusi na Uraine wangeweza kukubaliana rasmi kuruhusu usafirishwa wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi ifikapo wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/4E6kJ
USA UNO-Generalsekretär Antonio Guterres Ukraine
Picha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aidha amesema baada ya mazungumzo hayo kwamba wana matarajio shughuli hiyo itarejea hivi karibuni, na pengine wiki ijayo.

"Leo huko Istanbul, tumeshuhudia hatua muhimu ya kuhakikisha usafirishaji salama wa bidhaa za chakula za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi. Katika ulimwengu uliogubikwa na kiwingu cha machafuko, leo, hatimaye, tuna mwanga wa matumaini." Alisema Guterres.

Soma Zaidi: Juhudi za kufungua njia za usafirishaji chakula zashika kasi

Guterres aidha amesema alikuwa katika makubaliano mapana kuhusu mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusafirisha mamilioni ya tani ya nafaka zilizozuiwa Ukraine kutokana na vita.

Mwenyeji wa mazungumzo hayo, waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulus Akar, alisema pande zilizoshiriki zimekubaliana juu ya udhibiti wa pamoja kwenye bandari na nafaka zitakazokuwa zikisafirishwa ili kuhakikisha usalama. Amesema anaamini makubaliano ya mwisho yatatangazwa wiki ijayo.

Na huko Amsterdam, mwendesha mashitaka wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu, ICC Karim Khan ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kujitoa kwa dhati katika kuyafungua mashitaka ya uhalifu wa kivita unaofanyika nchini Ukraine. Amesema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa unaojadili mashitaka ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine, mjini The Hague.

Niederlande ICC Gebäude Den Haag
Mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu imetoa mwito kwa jamii ya kimataifa kujizatiti katika kuhakikisha kesi za uhalifu wa kivita nchini Ukraine zinafunguliwa.Picha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Kamishna wa haki kwenye Umoja wa Ulaya Didier Reynders amezungumzia jukumu kubwa lililopo mbele yao akisema litahitaji pia mfumo imara wa mahakama wa Ukraine.

Zaidi ya mawaziri 30 na waendesha mashitaka kutoka Ulaya na mataifa mengine ya magharibi wanakutana mjini The Hague kujadiliana juu ya mkakati wa pamoja kufungua mashitaka ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine. Mkutano huo uliitishwa na kamisheni ya Ulaya, wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi na ofisi ya mwendesha mashitaka wa mahakama ya ICC.

Na huko Bali, waziri wa fedha wa Marekani Janeth Yellen amesema leo kwamba vita vya Urusi vinaibua changamoto kubwa kabisa kwenye uchumi wa ulimwengu, wakati mawaziri wa fedha wa kundi la G20 pamoja na magavana wa Benki kuu wakijiandaa kuanza mazungumzo nchini Indonesia, siku ya Ijumaa na Jumamosi.

Soma Zaidi: Mawaziri wa nje wa G20 kuanza mazungumzo, Bali

Mzozo huo umesababisha mfumuko wa haraka wa bei wakati dunia ilipambana kuzifufua chumi zake zilizoathiriwa na janga la UVIKO-19. Kulingana na makisio ya kamisheni ya Ulaya vita hivyo vitachochea mfumuko wa bei kwa hadi asilimia 7.6, ambacho ni cha juu kabisa kushuhudiwa ulimwenguni.

Yellen amesema ataendelea kuwahimiza wanachama wenzake wa G20 kwenye mkutano huo juu ya ukomo wa bei ya mafuta kutoka Urusi na kuongeza shinikizo kwa Moscow kumaliza vita na kupunguza gharama za nishati.

Mashirika: RTRE/DW