UN: Matamshi ya chuki yanachochea vita vya Ethiopia
20 Oktoba 2022Alice Wairimu Nderitu, mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na kuzuia mauaji ya halaiki, amesema katika taarifa yake jana kuwa kauli za uchochezi zinazotolewa na viongozi wa kisiasa na wale wa makundi yenye silaha katika mzozo wa Tigray "daima zinaendelea".
Nderitu ameendelea kuwa kuna kauli ambazo mara nyingi huenezwa kupitia mitandao ya kijamii, na ambazo hudhalilisha watu kwa kuwafananisha na "virusi" au "saratani", ambavyo vinapaswa kutokomezwa na hivyo kutoa wito wa mauaji ya kila kijana wa Tigray, jambo ambalo amesema ni hatari sana.
Mapigano yalizuka tena mwezi Agosti kati ya vikosi vya Tigray na vile vya serikali, na kuvunja makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa mwezi Machi na ambayo yaliruhusu msaada muhimu kuwasilishwa katika eneo hilo.
Soma zaidi: Muungano wa Afrika waandaa mazungumzo ya amani Ethiopia
Mapigano yameongezeka katika wiki za hivi karibuni wakati wanajeshi wa serikali ya Addis wakijaribu kuchukua udhibiti wa miji ya Tigray. Mapema wiki hii walichukua udhibiti ya miji mitatu, ikiwa ni pamoja na mji wa Shire. Wanajeshi wa Eritrea wanaunga mkono jeshi la Ethiopia.
Mzozo wachochea njaa
Ugavi wa misaada unatatizwa na ukosefu wa mafuta na kukatika kwa mawasiliano huko Tigray. Shirika la habari la AP liliripoti Jumamosi kwamba Timu ya Umoja wa Mataifa iligundua vifo vya watu 10 vinavyohushwa na njaa katika kambi saba za wakimbizi wa ndani kaskazini magharibi mwa Tigray.
Soma zaidi:UN: Hali ya vita vya Tigray inazidi kuwa mbaya zaidi
Mzozo huo, ulioibuka karibu miaka miwili iliyopita, umeenea kutoka Tigray hadi katika mikoa ya jirani ya Afar na Amhara.
Mkuu wa Umoja wa Afrika na Katibu mkuu wa Umoja wa Matifa wanazitaka pande zinazozozana kusitisha mapigano na kuanzisha mazungumzo ya amani ambayo yalitarajiwa kuanza mapema mwezi huu nchini Afrika Kusini, lakini yalicheleweshwa kwa sababu za kiufundi.
Mzozo waendelea kukua
Alice Wairimu Nderitu amesema kumekuwa kukishuhudiwa viwango vya kutisha vya matamshi ya chuki na uchochezi na kwamba mgogoro huo umefikia viwango vipya vya vurugu na vya kutisha, hasa kuenea kwa ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia.
Mshauri huyo wa Umoja wa Matifa ameendelea kuwa unyanyasaji wa kikatili unaofanyika unachochewa na msururu wa matamshi ya chuki na ya kikabila ambayo yanaenezwa mtandaoni, na kuzitaka kampuni za teknolojia na mitandao yao ya kijamii, kutumia zana zote walizo nazo ili kukomesha kuenea kwa matamshi ya chuki yanayo jumuisha uchochezi, ubaguzi na hata uadui.
Mamilioni ya watu huko Tigray, Amhara na Afar wametimuliwa katika makazi yao huku maelfu ya wengine wakiaminika kuuawa katika mzozo huo ulioanza Novemba mwaka 2020.