1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuafikiana kuhusu Misri

Admin.WagnerD21 Agosti 2013

Maafisa wa usalama Misri wamewakamata viongozi wengine wawili wa udugu wa kiislamu huku kukiwa na uwezekano wa kuachiwa huru Rais wa zamani Hosni Muabarak na umoja wa Ulaya ukikutana juu uhusiano wake na Misri

https://p.dw.com/p/19Twv
Picha: Reuters

Duru za kijeshi zimearifu kuwa mhubiri wa udugu wa kiislamu Safwat Hegazy amekamatwa karibu na mpaka wa Misri na Libya magharibi mwa nchi hiyo. Hegazy amekuwa akijificha tangu kibali cha kukamatwa kwake kutolewa mwezi uliopita baada ya Rais Mohammed Mursi kung'olewa madarakani.

Msemaji wa tawi la kisiasa la udugu wa kiislamu chama cha uhuru na haki, Mourad Ali naye amekamatwa katika uwanja wa ndege wa Cairo alipokuwa akijaribu kuabiri ndege ya kuelekea Italia.Duru kutoka uwanja huo wa ndege zimesema Ali ambaye yuko kwenye orodha ya watu wasioruhisiwa kusafiri kutoka Misri,alikuwa amenyoa ndevu na kuvalia mavazi ya kawaida.

Kukamatwa kwa maafisa hao wawili kunakuja siku moja baada ya kiongozi wao Mohammed Badie kukamatwa.

Je Mubarak ataachiwa?

Huku hayo yakijiri,Rais wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak huenda akaachiliwa huru baada ya mahakama leo kutathimini kesi dhidi yake,na kuzua uwezekano wa kuchochea zaidi mzozo wa kisiasa nchini Misri.

Rais wa zamani Hosni Mubarak
Rais wa zamani Hosni MubarakPicha: picture-alliance/dpa

Mahakama inapangiwa kufanya kikao chake katika jela anakozuiliwa Mubarak leo na kutathimini ombi lililowasilishwa na wakili wake wa kutaka kiongozi huyo aliyeng'olewa madarakani mwaka 2011 kuachiliwa huru.

Iwapo mahakama itakubali ombi hilo, kutakuwa hakuna sababu ya kuendelea kuzuiliwa kwake licha ya kuwa amefunguliwa tena mashitaka ya kutochukua hatua muafaka za kuzuia mauaji wakati wa wimbi la uasi lililomng'oa madarakani.

Mubarak mwenye umri wa miaka 85 huenda asiwe na mashiko ya kisiasa tena lakini kuachiliwa kwake kunabashiriwa kuibua maswali ya iwapo wimbi hilo la uasi ambalo lilitia kikomo utawala wake wa miaka 30 limesababisha muundo mpya wa serikali ya kijeshi.

Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels kuijadili Misri na kutathimini msaada wanaotoa kwa nchi hiyo wa euro bilioni 6.7 kila mwaka.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Catherine Ashton
Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Catherine AshtonPicha: Reuters

Mawaziri hao 28 wataangalia mapendekezo ya mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Bi Catherine Ashton ambaye ana mawasiliano ya mara kwa mara na pande zote mbili katika mzozo wa Misri ili kuona iwapo wataweza kuwabinya viongozi wa Misri kuafikia suluhu la kisiasa.

Umoja wa Ulaya kuibinya Misri

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema lengo la umoja huo ni kuhakikisha pande zote zinarejea katika meza ya mazungumzo na kuepusha Misri kuwa kitovu cha ugaidi.

Tayari Ujerumani na Italia zimesitisha biashara ya silaha na Misri Huku Denmark nayo ikisitisha ufadhili wa miradi ya maendeleo kwa mashirika ya serikali.

Saudi Arabia imeutaka ulimwengu kuiunga mkono serikali ya muda ya Misri ili iweze kuafikia udhabiti na kutotatiza juhudi hizo.Waziri wa mambo ya nje wa Saudia, Saud al Faisal amesema wanatarajia jamii ya kimataifa kuunga mkono juhudi za Misri za kurejesha usalama,udhabiti na ufanisi.Saudi Arabia imetangaza nchi za kiarabu ziko tayari kuipa Misri misaada iwapo mataifa ya magharibi yatasitisha ufadhili wao.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Yusuf Saumu