Udugu wa Kiislamu wapanga maandamano zaidi
18 Agosti 2013Waandamanaji watakusanyika karibu na mahakama ya katiba kusini mwa mji wa Cairo.
Waungaji mkono wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi wanapanga kufanya maandamano mengine mjini Cairo leo Jumapili(18.08.2013), na kuongeza hofu ya umwagikaji zaidi wa damu baada ya mamia ya watu kuuwawa wiki hii.
Kundi la Udugu wa Kiislamu kufutwa kisheria
Maandamano hayo yanakuja wakati serikali inatafakari kulivunjia kabisa kisheria kundi la Udugu wa Kiislamu na waendesha mashtaka wanawahoji wafuasi 250 wa Mursi kuhusiana na mauaji na madai ya ugaidi.
serikali inawashutumu viongozi wa makundi ya Kiislamu kwa kuchochea ghasia na imeahidi kupambana na kile ilichokiita , "nguvu za ugaidi na uharibifu".
Ghasia zilianza siku ya jumatano wakati majeshi ya usalama yalipowaondoa kwa nguvu waandamanaji katika maeneo mawili makubwa ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi mjini Cairo. Kiasi ya watu 750 wameuwawa katika hatua hiyo ya jeshi pamoja na ghasia zilizofuatia nchi nzima.
Hatua ya jeshi kumuondoa madarakani Mursi , Julai 3 mwaka huu , baada ya maandamano ya mamilioni ya Wamisri wakidai ajiuzulu, imewagawa kwa kiasi kikubwa Wamisri , ambalo ni taifa lenye wakaazi wengi miongoni mwa mataifa ya Kiarabu.
Shutuma kali
Ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wa makundi ya Kiislamu umesababisha shutuma kali kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, hususan kutoka bara la Ulaya na Marekani. Hata hivyo , mataifa ya ghuba yameeleza kuunga kwao mkono watawala wa mpito nchini Misri.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema jana jumamosi (17.08.2013) kuwa anashtushwa na maandamano yenye ghasia pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi ya polisi.
Ban amewataka waandamanaji mitaani na maafisa kuwa na uvumilivu wa hali ya juu na kuelekea haraka katika kupunguza ghasia hizo. Wakati huo huo polisi ya Misri imewaondoa waandamanaji wa Kiislamu kutoka katika msikiti mjini Cairo jana Jumamosi baada ya mapambano ikiwa ni pamoja na kurushia risasi, wakati idadi ya vifo katika siku hizo nne za machafuko ikifikia 750.
Majeshi ya usalama yaliwaondoa waungaji mkono wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi kutoka msikiti wa Al-Fath, huku kundi kubwa la watu wenye hasira likijaribu kuwapiga watu hao wakiwaita magaidi.
Mapambano hayo yamekuja wakati serikali ikisema kuwa watu 173 wameuwawa katika muda wa saa 24 zilizopita , na kufikisha idadi ya watu waliouwawa nchi nzima kufikia 750 tangu siku ya Jumatano, wakati polisi walipowaondoa waandamanaji kwa nguvu katika makambi mawili ya watu wanaomuunga mkono Mursi katika mji mkuu.
Kwingineko nchini Misri baada ya kuchoma moto shule ya watawa wa Franciscan , waislamu waliwatembeza watawa wawili wa kike barabarani kama "wafungwa wa kivita" kabla ya mwanamke mmoja Muislamu kuomba kuwapa hifadhi. Wanawake wengine wawili waliokuwa wakifanyakazi katika shule hiyo walishambuliwa kingono na kutukanwa wakati wakijaribu kupita katika kundi la watu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / dpae
Mhariri : Amina Abubakar