1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Diplomasia yashika kasi Misri

Admin.WagnerD1 Agosti 2013

Wafuasi wa rais aliyepinduliwa nchini Misri, wameapa kuendeleza maandamano licha ya amri ya kuwakandamiza, huku wanadipolomasia wakijaribu kutafuta suluhu ili kukomesha mgogoro uliyozidi kuigawa nchi.

https://p.dw.com/p/19I9m
Außenminister Guido Westerwelle (FDP) sitzt gegenüber seines ägyptischen Amtskollegen Nabil Fahmy am 01.08.2013bei einem Gespräch im Außenministerium in Kairo in Ägypten. Westerwelle hält sich zu politischen Gesprächen in Kairo auf und will unter anderem mit dem Präsidenten der Übergangsregierung Mansour zusammentreffen. Foto: Michael Kappeler/dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++ FREI FÜR SOCIAL MEDIA
Guido Westerwelle in Ägypten 01.08.2013Picha: picture-alliance/dpa

Wafuasi wa rais Muhammad Mursi wamesema watafanya maandamano ya watu milioni moja siku ya Ijumaa, na kulaani mamlaka iliyopewa kwa jeshi la polisi na utawala wa muda kukomesha maandamano yao kwa kutumia nji zote.

Juhudi za kidiplomasia zimeshika kasi, ambapo mjumbe wa Umoja wa Ulaya katika mashariki ya kati na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle, wote wakiwasili mjini Cairo kuzihimiza kambi pinzani kuepuka umuagaji damu na kutafuta suluhu ya muafaka. Jumuiya ya kimataifa, ambayo ilielezea wasiwasi kuhusu vurugu zilizofuatia kupinduliwa kwa rais Mursi Julai 3, imeonya dhidi ya umuagaji zaidi wa damu nchini humo.

Heshimuni haki ya maandamano
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imetowa wito kwa serikali ya muda kuheshimu haki ya mikusanyiko ya amani, ambayo msemaji wa wizara hiyo Marie Harf, aliwaambia waandishi wa habari kuwa inahusisha migomo. Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague, katika mazungumzo kwa njia ya simu na makamu wa rais wa muda Mohamed ElBaradei, alitoa wito wa kukomesha haraka umuagaji damu, na kuachiwa mara moja kwa rais Mursi.

Wafuasi wa Mursi wakiwa katika kivuli cha hema mjini Cairo.
Wafuasi wa Mursi wakiwa katika kivuli cha hema mjini Cairo.Picha: picture-alliance/AP

Jumatano mchana, serikali ya muda ilitangaza kulipa mamlaka jeshi la polisi nchini Misri kutumia njia zote kukomesha migomo na maandamano ya wafuasi wa Mursi, ikisema kuendelea kwa migomo hiyo kunatishia usalama wa taifa. Amri hiyo ilizua hofu ya kutokea kwa vurugu zaidi, ikiwa ni chini ya wiki moja tangu kuuawa kwa watu 82 katika machafuko yaliyotokea katika mkutano wa wafuasi wa Mursi mjini Cairo.

Wafuasi wa Mursi waliokuja pamoja katika Muungano wa kutetea uhalali na kupinga mapinduzi wamelaani wito wa serikali kukandamiza maandamano yao, na kuwasihi maafisa wa polisi na jeshi kutokubali wito wa kuwageuzia silaha ndugu zao Wamisri. Shirika la kuteteta haki za binaadamu la Amnesty International nalo limelaani amri iliyotolewa na serikali ya muda, na Mkurugenzi wake Kenneth Roth aliandika katika mtandao wake wa Twitter, kuwa maandamano ya amani siyo tishio kwa usalama wa taifa.

Westerwelle ahimiza maelewano
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle, ambae aliwasili mjini Cairo jana Jumatano, alizisihi pande zote kuendelea kuwa watulivu na kutafuta suluhusu inayojumuisha watu wote. Westerwelle alitarajiwa kuungana na Mjumbe wa Umoja wa Ulaya Bernardino Leon, ambae anaendeleza juhudi za kidiplomasia zilizoanzishwa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Catherine Ashton, aliekuwa nchini humo kwa siku tatu.

Wafuasi wa Mursi katika uwanja wa Rabaa Adawiya.
Wafuasi wa Mursi katika uwanja wa Rabaa Adawiya.Picha: Reuters/Mohamed Abd El Ghany

Zaidi ya watu 250 wameuawa tangu jeshi lilipompindua Mursi, kufuatia maandamano ya nchi nzima. Wasiwasi uliongezeka kufuatia jana, baada ya vyanzo vya mahakama kudokeza kuwa viongozi kadhaa wa Udugu wa Kiislamu watapelekwa mahakamani kushtakiwa kwakuchochea mauaji.

Kiongozi wa kidini wa Udugu huo, ambae yuko mafichoni Mohammad Badie, na makamu wake wawili, Khairat al-Shatar na Rashad Bayoumi wanatuhumiwa kwa kuchochea mauaji ya waandamanaji nje ya makao makuu ya Udugu wa Kiislamu usiku wa Juni 30. Mursi mwenyewe amewekwa rumande kwa madai kuwa alitoroka gerezani wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyomuondoa rais Hosni Mubarak.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Josephat Charo