1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wawakosowa viongozi wa dunia kwenye COP28

6 Desemba 2023

Mkuu wa Ofisi ya Tabianchi ya Umoja wa Mataifa, Simon Stiell, ameyatuhumu mataifa kwa "kuoneshana ushindani" katika mazungumzo ya COP28 yanayoendelea mjini Dubai.

https://p.dw.com/p/4ZqIX
Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi, Simon Stiell.
Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi, Simon Stiell.Picha: Bebeto Matthews/AP Photo/picture alliance

Stiell amewashinikiza wapatanishi wanaobishana kuhusu suala tete la nishati ya visukuku kuhakikisha wanapata makubaliano yenye manufaa kwa sayari ya dunia.

"Kama tunataka kuokoa maisha na kutimiza lengo la kupunguza viwango vya nyuzijoto hadi 1.5, matokeo ya COP lazima yapewe umuhimu mkubwa. Mwishoni mwa wiki ijayo, tunahitaji COP kutupatia chombo kinachoweza kuharakisha hatua za udhibiti wa uchafuzi wa mazingira. Kwa sasa tupo kwenye chombo kizee kinachokimbia kwenye reli mbovu. Nyenzo zote zipo." Alisema mkuu huyo wa Ofisi ya Tabianchi ya Umoja wa Mataifa.

Soma zaidi: COP28: Mazungumzo ya matumizi ya nishati ya visukuku yapamba moto

Shinikizo linaongezeka wakati wiki ya kwanza ya mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Mataifa ukiongozwa na Umoja wa Falme za Kiarabu ikielekea mwishoni.

Nalo Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa barani Ulaya limethibitisha kuwa mwaka wa 2023 ndio utakaokuwa na joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia.

Rasimu ya karibuni kabisa ya makubaliano ya kimataifa ya tabianchi inatarajiwa kutolewa leo kabla ya kukamilishwa kwa mkutano huo mnamo Desemba 12 kwa mujibu wa vyanzo kwenye mkutano huo.

Hatima ya nishati za mafuta, gesi na makaa ya mawe - ambazo zinasababisha ongezeko la joto duniani - imekuwa suala tete kwenye mazungumzo hayo, na migawanyiko kuhusu mustakabali wa nishati hizo umeugubika vikao vinavyoendelea.