Umoja wa Mataifa waonya dhidi ya mripuko wa maambukizo Libya
19 Septemba 2023Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ulisema ulikuwa na wasiwasi hasa kuhusu uchafuzi wa maji na ukosefu wa vyoo baada ya mabwawa mawili kubomoka wakati wa Kimbunga Daniel na kusababisha mafuriko makubwa.
Mashirika tisa yanayoshughulikia maafa hayo yanafanya juhudi za kuzuwia magonjwa kuongezeka na kusababisha janga jingine katika nchi hiyo ambayo tayari imeshasambaratishwa kwa vita vya takribani muongo mzima.
Soma zaidi: UN yatahadharisha kuhusu hali ya mabwawa mengine 2 Libya
Manusura wa mafuriko Libya wakabiliwa na uhaba wa maji safi
Libya, ambayo iliwahi kujitegemea kwa huduma zote muhimu kabla ya kupinduliwa na kuuawa kwa kiongozi wake, Muammar Gaddafi, inapokea tani 28 za vifaa vya matibabu kutoka katika Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Mkuu wa Kituo cha Kupambana na Magonjwa nchini humo, Haider al-Saeih, alisema takribani watu 150, kati yao watoto 55, wamepatwa na ugonjwa wa kuharisha baada ya kunywa maji machafu katika mji uliokumbwa vibaya na mafuriko, Derna.