Umoja wa Mataifa walaani kukamatwa wanasheria Tunisia
17 Mei 2024Umoja wa Mataifa leo umelaani hatua ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa mawakili nchini Tunisia, ukisema kuwekwa kizuizini kwa watu hao wanaowajumuisha waandishi habari na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kunadhoofisha utawala wa sheria nchini humo.
Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA Ravina Shamdasani, amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba uvamizi ulioripotiwa wiki iliyopita dhidi ya Chama cha Wanasheria wa Tunisia unakiuka viwango vya kimataifa kuhusu ulinzi wa uhuru na majukumu ya mawakili.
Soma: Mwanaharakati wa Tunisia Khayam Turki akamatwa na polisi
Shamdasani ameongeza kuwa mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amezihimiza mamlaka kuheshimu na kulinda haki ya kujieleza na kukusanyika kwa amani.
Msemaji huyo ameendelea kusema utawala wa sheria lazima udumishwe, na wale waliowekwa kizuizini kiholela, ikiwa ni pamoja na wale wanaotetea haki za wahamiaji na vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, kuachiliwa huru.