1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wakubali uchunguzi wa pamoja Tigray

Josephat Charo
18 Machi 2021

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia haki za binadamu Michelle Bachelet ameridhia ombi la Ethiopia kufanya uchunguzi wa pamoja katika eneo linalokabiliwa na vita la Tigray, kaskazini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3qmno
Michelle Bachelet | UN Hochkommissarin für Menschenrechte
Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Msemaji wa afisi ya shirika la Hakiza binadamu la Umoja wa Mataifa, Jonathan Fowler, amesema Bachelet amekubali ombi la shirika la kitaifa la haki za binadamu la Ethiopia kufanya uchunguzi wa pamoja Tigray.Akizungumza jana mjini New York, Fowler amesema wanaandaa mpango wa pamoja unaojumuisha raslimali zitakazohitajika na utaratibu mzima ili kuanzisha tume hizo haraka iwezekanavyo.

Mapigano kati ya majeshi ya serikali na chama tawala cha zamani cha eneo hilo, chama cha ukombozi cha watu wa Tigray, TPLF, yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimu mamia kwa maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao katika eneo la milima lenye wakazi takriban milioni tano.

Miezi minne tangu mzozo wa Tigray kuanza kati ya majeshi ya serikali na chama cha ukombozi cha watu wa Tigray, mamia kwa maalfu ya watu wameachwa bila makazi na maelfu zaidi wamekufa. Mpaka sasa haijabainika wazi ni raia wangapi hasa waliouliwa katika mzozo huo. Inakadiriwa watu 500,000 wamepoteza makazi yao na maafisa wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu wanahofia idadi kubwa ya watu inayoendelea kuongezeka huenda wanakosa chakula na wanakufa kwa njaa huko Tigray. Mapigano yalizuka wakati wa mavuno ulipokaribia katika eneo ambalo kwa kiwango kikubwa hutegemea kilimo na kuwalazimisha watu wengi kuzikimbia nyumba zao.

Hali ya wakaazi ni ngumu

Wakazi wa vijiji vya Mayweini na Cheli, vilivivyoko karibu na mji mkuu wa Tigray, Mekelle, wameelezea jinsi walivyoshuhudia vifo vya watoto wakati wa mapigano hayo. Picha za video kutoka vijiji hivyo zimeonyesha magari ya jeshi yaliyochomwa kwa moto, majengo yaliyoharibiwa, maganda ya risasi ardhini na makaburi yaliyochimbwa hivi karibuni.

BG Tigray | Denglat
Wahanga wa Tigray walizikwa kwenye makaburi ya pamoja kama hiliPicha: Maria Gerth-Niculescu/DW

Mapigano hayo yalimlazimu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Anthony Blinken kutamka wiki iliyopita kwamba kinachoendelea Tigray ni mauaji ya safisha safisha ya kikabila, ikiwa ni mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi ya juu katika jumuiya ya kimataifa kuelezea waziwazi namna hiyo mauaji ya Tigray. Serikali ya Ethiopia imekanusha madai hayo ya mauaji ya kimbari Tigray ikisema hayana msingi wowote.

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu mauaji yanayofanywa katika eneo la Tigray. Jumamosi iliyopita wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia ilisema iko tayari kushirikiana na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kufanya uchunguzi kuhusiana na madai hayo.

Mwezi uliopita shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International liliituhumu Eritrea kwa kuwaua mamia ya raia katika kipindi cha masaa 24 katika mji wa Axum mwaka uliopita. Eritrea ilikanusha madai hayo, lakini tume ya kitaifa ya haki za binadamu ya Ethiopia pia imeelezea juu ya mauaji hayo katika hatua isiyo ya kawaida ya kukiri kutoka kwa upande wa serikali kwamba wanajeshi wa Eritrea wamejipenyeza katika mzozo wa Tigray.

Umoja wa Mataifa na Marekani zimekanusha madai ya kuwepo majeshi ya Eritrea Tigray, licha ya maelezo yanayotolewa na watu walioshuhudia kwamba Waeritrea wapo.

(reuters,aptn)