Serikali Ethiopia yashinikizwa kuondoa vikosi vyake Tigray
11 Machi 2021Ukosoaji wa mienendo ya vikosi vya serikali pamoja na washirika wake katika nchi jirani ya Eritrea, ulizidi kutokea baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken kusisitiza hapo jana kwamba mauaji ya kikabila yalitokea katika baadhi ya sehemu mjini Tigray.
Akizungumza na kamati ya mambo ya kigeni katika Baraza la Wawakilishi nchini Marekani, Blinken amesema changamoto iliyopo nchini Ethiopia ni ngumu kuikabili, na ni moja ya kitu Marekani inachokipa kipaumbele hasa hali ilivyo mjini Tigray, kunakoendelea kuripotiwa visa vya uvunjifu wa haki za binaadamu, mateso na ukatili.
soma zaidi: HRW: Mashambulizi yasababisha vifo vya watu wengi katika siku za mwanzo za vita Tigray
Licha ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abby Ahmed kuelezea wasiwasi wake kuhusu matendo ya viongozi wa Tigray, Blinken amesema hali ilivyo kwa sasa katika eneo hilo haikubaliki na lazima isitishwe. Amesema ni muhimu kuhakikisha wafanyakazi wa misaada ya kiutu wanafika huko kuhakikisha watu wake wanapata huduma muhimu na wanalindwa.
Blinken amesema vikosi vya Eritrea pamoja na wapiganaji kutoka Amhara eneo linalopakana na Tigray, wanapaswa kuondoka huko huku akisisitiza kuwa eneo hilo linahitaji maafisa wa usalama wanaoheshimu haki za binaadamu na wala sio wale wanaoshiriki vitendo vya mauaji ya kikabila yalioonekana Magharibi mwa mji huo.
Hata hivyo hakuna maoni yoyote yaliyotolewa na serikali ya Ethiopia juu ya matamshi ya Blinken.
Viongozi wa Tigray wadai serikali ya Abby inatenda mauaji ya halaiki dhidi ya watu wake
Kwa upande wake Getachew Reda mmoja ya viongozi wa Tigray ametoa taarifa ya kulaani kile alichokiita kampeni ya mauaji ya halaiki dhidi ya watu wake. Taarifa hiyo imesema maelfu ya wakaazi wameuwawa, maelfu wengine kukosa makazi na mifumo ya miundo mbinu na mawasiliano imeharibiwa vibaya.
Taarifa hiyo iliyotumwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter imesema badala ya Abby Ahmed kukubali misaada ya kiutu kufika katika eneo hilo na kukubali pia wachunguzi wa kimataifa kuchunguza madai ya uhalifu, utawala wake pamoja na washirika wake wameendelea kushiriki vitendo vya uhalifu dhidi ya binaadamu katika wiki na siku za hivi karibuni.
soma zaidi: Mgogoro wa Tigray kudhoofisha utulivu nchini Ethiopia
Huku hayo yakiarifiwa mwanadiplomasia wa juu katika ubalozi wa Ethiopia nchini Marekani Berhane Kidanemariam alijiuzulu akisethiopian troops abbyema Abby ni kiongozi asiyejali na anaeligawa taifa lake.
Mapigano nchini Ethiopia yalianza mwezi Novemba mwaka jana wakati Abby alipotuma vikosi vya serikali kuu mjini Tigray baada ya kambi ya kijeshi ya serikali kuu kushambuliwa. Hadi sasa hakuna anayejua ni watu wangapi hasa waliouwawa katika mapigano hayo.
Maafisa wa misaada ya kiutu wameonya kuwa watu wengi zaidi huenda wakafa njaa katika eneo hilo la Tigray.
Chanzo: ap