Mgogoro wa Tigray kudhoofisha utulivu nchini Ethiopia
4 Februari 2021Mkuu wa Masuala ya Kibinaadamu na Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock ameliambia Baraza la Usalama kuwa mgogoro wa mkoa wa Tigray nchini Ethiopia huenda ukaudhoofisha zaidi utulivu nchini humo, wakati akionya kuwa hali mbaya kabisa ya kiutu katika eneo hilo la kaskazini inatarajiwa kuwa mbaya hata zaidi. Lowcock amesema kuna ripoti za kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kwingineko, hali ambayo huenda ni kutokana na ombwe lililosababishwa na kutumwa upya kwa wanajeshi wa Ethiopia katika jimbo la Tigray. Mamia ya maelefu ya watu mkoani Tigray hawajapokea msaada na Umoja wa Mataifa umeshindwa kuitathmini hali hiyo kwa sababu maafisa wake hawawezi kuingia katika eneo hilo bila vikwazo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali ya mkoa huo.