Jeshi la Sudan na RSF kurejea kwenye mazungumzo
26 Oktoba 2023Jeshi la Sudan pamoja na kikosi cha Dharura, RSF wamesema wanarejea kwenye mazungumzo yaliyoanzishwa na Marekani na Saudi Arabia mjini Jeddah hii leo, wakati vita baina yao vilivyodumu kwa miezi sita vikiendelea kuligubika taifa hilo.
Jeshi la Sudan jana Jumatano lilikubali mwaliko huo kwa kuwa mazungumzo yanaweza kuwa njia moja wapo ya kumaliza mzozo, lakini limesema halitasitisha mapigano.
Kikosi cha RSF pia kimekubali kuhudhuria, ingawa jana Jumatano kilichapisha video iliyoonyesha msaidizi wa kiongozi wao, akiongoza wanajeshi katika eneo la Nyala, ambako ndiko kitovu cha vita.
Mapigano baina ya vikosi hivyo yalianza katikati ya mwezi Aprili na kusababisha kile ambacho mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths anaelezea kuwa ni mzozo mbaya kabisa wa kiutu katika historia ya hivi karibuni.