Ulimwengu walaani mapinduzi Sudan
26 Oktoba 2021Mapinduzi hayo, ambayo yamelaaniwa na Umoja wa Mataifa, Marekani na Umoja wa Ulaya yamekuja ikiwa ni zaidi ya miaka miwili baada ya waandamanaji kulazimisha kuondolewa kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu aliyeongoza kwa mkono wa chuma Omar al-Bashir na wiki chache tu kabla ya jeshi kukabidhi kwa raia uongozi wa baraza linaloongoza nchi hiyo.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kuandaa mkutano wa dharura baadae leo kuhusu mapinduzi ya Sudan. Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ireland, Norway na Estonia ziliomba mazungumzo ya dharura kuhusu hali inayoendelea Sudan.
Baada ya matukio ya jana alfajiri ya kukamatwa Waziri Mkuu Abdalla Hamdok na maafisa wengine waandamizi wa serikali, maelfu waliingia mitaani katika mji mkuu Khartoum, na mji pacha wa Omdurman kupinga hatua hiyo. Waliweka vizuizi barabarani na kuchoma moto matairi huku vikosi vya usalama vikitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya.
Duru zinasema watu saba wameuawa katika makabiliano hayo. Awali, Kamati ya Madaktari wa Sudan ilisema watu watatu walipigwa risasi na kuuawa na polisi huku wengine 80 wakijeruhiwa.
Soma zaidi: Yanayoendelea Sudan: Jeshi lavunja serikali ya mpito
Mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel-Fattah Burhan, alitangaza kwenye televisheni ya taifa kuwa anavunja serikali na Baraza Kuu Tawala, ambalo linajumuisha wanachama wa kijeshi na kiraia lililoundwa muda mfupi baada ya kuangushwa Bashir ili kuendesha nchi hiyo. Burhan alisema ugomvi miongoni mwa makundi ya kisiasa umesababisha uingiliaji wa kijeshi. Mivutano imekuwa ikiongezeka kwa wiki sasa kuhusu mkondo na mwendo wa mpito wa kuelekea demokrasia nchini Sudan. Jenerali hiyo alitangaza hali ya hatari na kusema jeshi litateuwa serikali ya wasomi kuiongoza nchi kuelekea uchaguzi unaopandwa Julai 2023. Lakini alisema wazi kuwa jeshi litasalia usukani.
Marekani imelaani vikali hatua hiyo ya kijeshi, na kutoa wito wa kurejeshwa haraka utawala wa kiraia na kuwachiwa huru kwa waziri mkuu aliyekamatwa.
Waziri wa Mambo ya Kigeni Antony Blinken amesema katika taarifa kuwa Marekani inapinga vikali hatua ya kuvunjwa serikali huku akielezea wasiwasi kuhusu ripoti kuwa vikosi vya usalama vinatumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji.
Serikali ya Marekani imesitisha utoaji wa msaada wa dharura wa kiuchumi wa dola milioni 700 kwa Sudan ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya serikali ya mpito.
Soma pia: Jeshi lawakamata mawaziri wanne Sudan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mapinduzi hayo ya kijeshi na vitendo vyote vinavyoweza kuhujumu kipindi cha mpito na utulivu nchini Sudan. Msemaji wake Stephane Dujarric amesema Guterres pia ametoa wito wa kuachiwa huru kwa maafisa wa serikali. Wito sawa na huo umetolewa na Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya ambapo mkuu wake wa sera za kigeni Joseph Borrell alisema anafuatilia matukio hayo kwa wasiwasi mkubwa.
Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameonya kuwa Sudan huenda ikarudi nyuma, akilihimiza jeshi kuwaachia huru maafisa waliokamatwa, lijionde mitaani na kutatua tofauti zao na serikali ya mpito kupitia mazungumzo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters