Yanayoendelea Sudan: Jeshi lavunja serikali ya mpito
25 Oktoba 2021Kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametoa tangazo hilo kupitia hotuba yake kwa njia ya Televisheni, kwamba serikali ya mpito ya Sudan imevunjwa. Al-Burhan ameongeza kuwa hatua hiyo ilikuwa muhimu kutokana na "vurugu za hivi karibuni" nchini Sudan.
Kulingana na kiongozi huyo, jeshi sasa litajaribu kuirejesha nchi katika mkondo wa demokrasia na kukabidhi mamlaka kwa serikali ya kiraia baada ya uchaguzi wa Julai mwaka 2023.
"Kuanzia leo sote tufanye kazi hadi uchaguzi mkuu wa Julai 2023 ili kuboresha maisha ya watu na kuwahakikishia ulinzi na usalama, pamoja na kuweka mazingira mwafaka ya vyama vya siasa ili kufikia tarehe maalum ya uchaguzi wakati watakapokuwa tayari zaidi."
Muungano mkuu wa upinzani nchini humo umeitisha uasi wa kiraia na maandamano kote nchini kufuatia tangazo la jeshi kuvunja serikali ya mpito. Muungano wa vikosi huru na mabadiliko, umelitaka baraza la kijeshi kujiuzulu na kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia. Pia limetaka kuachiwa kwa wanachama wote wa baraza la mawaziri na baraza huru, ambalo lilikuwa ndio chombo kinachotawala kikishirikiana mamlaka baina ya jeshi na raia hadi kilipovunjwa leo.
Duru zaidi zinasema kwamba maelfu ya waandamanaji wameingia katika mitaa ya mji wa Khartoum kupinga hatua ya jeshi kutwaa mamlaka. Waandamanaji walifanikiwa kuvuka vizuizi vya kiusalama vilivyowekwa na kuelekea makao makuu ya jeshi mjini Khartoum. Vurugu zimezuka mjini Khartoum wakati askari walipowafyatulia risasi watu waliomiminika mitaani. Vurugu hizo kwa kiasi kikubwa zimeripotiwa nje ya makao makuu ya jeshi. Huduma za intaneti zimeendelea kutatizika baada ya kuzimwa huku watu kadhaa wakiripotiwa kujeruhiwa kulingana na Tume kuu huru ya Madaktari wa Sudan.
Jumuiya ya kimataifa imeendelea kutoa miito ya kulaani hatua hiyo. Mwenyekiti ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema viongozi wa kisiasa wa Sudan wanapaswa kuachiwa huru na haki za binadamu kuheshimiwa. Katika taarifa yake, Mahamat ameongeza kuwa "mazungumzo ndio njia pekee ya kuokoa nchi na kipindi chake cha mpito cha demokrasia".
Wizara ya habari, awali ilisema kwamba waziri mkuu Abdala Hamdok alipelekwa eneo lisilojulikana. Hamdok alikataa kuunga mkono mapinduzi na badala yake akaitisha maandamano ya mtaani. Wajumbe wengine wa serikali pia nao wamekamatwa kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo.