Ulaya yaondoa vikwazo vya silaha kwa waasi Syria
28 Mei 2013Makubaliano hayo yalifikiwa usiku wa kuamkia leo baada ya mazungumzo magumu ya saa 12 mjini Brussels. Baada ya muafaka kupatikana, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague alisema waasi wa Syria wameondolewa vikwazo vya silaha, huku vikwazo vikali vikibakizwa kwa serikali ya rais Bashar al-Assad. Yasingefikiwa makubaliano mapya, muda wa vikwazo hivyo ambavyo ni pamoja na kushikiliwa kwa mali za rais Assad na maafisa wanaomuunga mkono ungemalizika Ijumaa usiku.
Ujumbe mzito kwa Assad
William Hague amewaambia waandishi wa habari kuwa makubaliano yaliyofikiwa yanatuma ujumbe mzito kwa serikali ya mjini Damascus.
''Ni muhimu kuonyesha kwamba tuko tayari kubadilisha vikwazo vya silaha, ili kuipelekea serikali ya rais Assad ujumbe usio na utata kwamba analazimika kujiunga na meza ya mazungumzo.'' Alisema Hague.
Msemaji wa mfungamano wa waasi aliyeko mjini Istanbul Kheled al Saleh amekaribisha uamuzi wa Umoja wa Ulaya, akisema huu ni wakati ambao wamekuwa wakiusubiri kwa hamu.
Licha ya makubaliano hayo lakini, mgawanyiko katika Umoja wa Ulaya kuhusu uamuzi huo umejidhihirisha wazi. Uingereza na Ufaransa zilipigia debe kuondolewa kwa vikwazo vya silaha kwa waasi, lakini Austria, Sweden, Finland na Jamhuri ya Czeck zilipinga hatua ya kurundika silaha zaidi katika mgogoro ambao tayari umegharimu maisha ya watu 94 elfu.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Austria Michael Spindelegger ambaye kwa muda mrefu amepinga kuwapa silaha zaidi waasi wa Syria, amesema hatua hiyo ni kinyume na maadili ya ulaya, ambayo ni jamii ya amani.
Ujerumani kusaka muafaka
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema nchi yake itajaribu kusaidia Ulaya kupata mtazamo sawa.
''Ni vigumu kujua wakati Ulaya itakazungumza kwa sauti moja kuhusu suala hili, lakini sisi Ujerumani tutafanya juhudi ili nchi zote wanachama ziwe na msimamo mmoja.'' Westerwelle alisema.
Afisa mmoja wa Ufaransa amesema kuwa uamuzi uliofikiwa ni wa kinadharia tu, kwani haitawezekana kutoa silaha zozote kwa waasi hao kabla ya tarehe moja mwezi Agosti. Kucheleweshwa huko kunalenga kutoa muda kwa mkutano unaoandaliwa na Urusi na Marekani uweze kufanyika, kwa matumaini kwamba waasi na serikali ya Syria watakuwa tayari kuhudhuria.
Makubaliano yaliyofikiwa yanatoa uhuru kwa kila nchi kuamua yenyewe kuwapa silaha waasi, lakini mawaziri wamekubaliana kuendelea kuheshimu sheria za Umoja wa Ulaya kuhusu uuzwaji wa silaha nje ya umoja huo.
Kuna wale walio na maoni kuwa kinachokosekana nchini Syria sio silaha. ''Tayari kuna silaha nyingi mikononi mwa watu wasio paswa kuwa nazo'', alisema waziri mkuu wa Uholanzi Frans Timmermans.
Juhudi sambamba
Wakati mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wakikutana Brussels, mkutano mwingine ulikuwa ukiendelea mjini Paris kati ya wenzao wa Marekani na Urusi kuzungumzia mkutano wa kimataifa wa amani unaoandaliwa na nchi hizo.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadaye, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema kuwa kuuandaa mkutano huo si jambo jepesi, ingawa aliongeza kuwa ipo nafasi ya kufanikiwa.
Mwenzake wa Marekani John Kerry ambaye alionya kuwa kuwa kadri pande mbili za mgogoro nchini Syria zinavyoendelea kuchelewa kuzungumza ndivyo hali itakavyozidi kuwa mabaya, amesema kuwa mkutano baina yake na Lavrov ulikuwa na mafanikio kwa kiasi fulani.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPEA
Mhariri: Ssessanga Iddi