Mrengo wa kushoto wa Ulaya wataka vita vya Ukraine kumalizwa
19 Machi 2024Baier aidha ameunga mkono wito wenye utata ulitolewa na kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis wa kuitaka Kyiv kujisalimisha. Anasema hayo wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiendelea kukutana na viongozi waandamizi wa Marekani ili kuangazia namna ya kuimarisha zaidi uhusiano kati ya mataifa hayo katikati ya vita hivyo.
Walter Baier, mwanasiasa kutoka nchini Austria amesema anaamini hakuna njia nyingine itakayofaa kuwasaidai watu wa Ukraine zaidi ya kuvimaliza vita, ingawa amesisitiza kwamba chama chake cha European Left kinachojumuisha vyama 26 vya siasa za kisoshalisti, kidemokrasia na kikomunisti katika Umoja wa Ulaya na nchi nyingine za Ulaya kinalaani vikali uvamizi wa Urusi kwenye ilani yake ya uchaguzi wa Ulaya utaofanyika mwezi Juni. Mwanasiasa huyo anawania kuiongoza Halmashauri Kuu ya Ulaya.
Ameviambia vyombo vya habari kwenye mahojiano siku ya Jumatatu kwamba anatamani Umoja Ulaya sasa ugeukie juhudi za kidiplomasia ili kufanikisha usitishwaji wa mapigano na hatimaye kuwaondoa wanajeshi wa Urusi na kuongeza kuwa anaunga mkono kikamilifu kile ambacho amekisema Papa Francis mapema mwezi huu na kutoa rai kwamba wakati umefika sasa wa kusitisha mauaji.
Zelensky akutana na Seneta wa Marekani, wajadilia ushirikiano zaidi
Huku hayo yakiendelea, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amefanya mazungumzo jana usiku na Seneta wa Republican wa nchini Marekani Lindsey Graham na kugusia namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya mataifa hayo.
"Tulizungumzia, pamoja na mambo mengine, kuhusu umuhimu wa uhuru na demokrasia kushinda katika vita hivi, hapa Ukraine, kwa sababu vinginevyo uchokozi na machafuko ya Urusi yataenea duniani kote. Nilimjulisha Seneta (Graham) kuhusu hali ya uwanja wa vita na mahitaji muhimu ya vikosi vyetu vya ulinzi.," alisema Zelensky.
Soma pia:Zelensky kufanya ziara nchini Uturuki na atakutana na Erdogan
Zelensky amesema amemwambia Seneta huyo wa North Carolina kwamba mahitaji hayo ni muhimu kwa vikosi vyake vinavyokabiliwa na uhaba wa silaha na vinavyohitaji karibu dola bilioni 48 ili kupata makombora na kuimarisha mifumo ya kujilinda.
Seneta Graham kwa upande wake amemueleza Rais Zelensky baada ya mazungumzo hayo kwamba kifurushi cha msaada kilichokwama katika Bunge la Marekani kitaidhinishwa hivi karibuni. Seneta huyo na wabunge wa Republican wameunga mkono wazo la mikopo badala ya ruzuku kwa washirika wa Marekani ili kuyafanya matumizi kuwa endelevu, mpango uliopendekezwa na Rais wa zamani Donald Trump, anayetarajiwa kugombea urais kupitia Republican kwenye uchaguzi wa mwaka huu wa urais.
Kwa upande mwingine, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amesema jana kwamba Ulaya kwa sasa inalazimika kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi na kuhamia kwenye "uchumi wa wakati wa vita" ili kukabiliana na kitisho kinachoibuliwa na Urusi.
Michel amesema hayo katika safu fupi ya maoni iliyochapishwa kwenye magazeti ya Ulaya na Tovuti ya Euractiv, kuelekea kikao cha viongozi waandamizi wa Ulaya siku ya Alhamisi kitakachojadili msaada kwa ajili ya Ukraine. Amesema Ulaya pia inahitajika kuwajibika kwa ajili ya usalama wake badala ya kutegemea zaidi msaada wa nchi kama Marekani. Ameuambia Umoja huo ya kwamba kama wanahitaji amani, wanatakiwa kujiandaa kwa vita.
Michel alizitaka nchi za Ulaya kuhakikisha Ukraine inakipata kile inachokihitajika kwenye uwanja wa vita na kuyaomba mataifa wanachama kuwezesha uwekezaji katika ulinzi. Mataifa hayo yaliidhinisha makubaliano siku ya Jumatatu ya kuongeza msaada wa yuro bilioni 5 kwa ajili ya vikosi vya Ukraine.