1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yawaomba washirika wa NATO kuharakisha silaha

Hawa Bihoga
15 Februari 2023

Ukraine imewataka washirika wake kuharakisha msaada wa kijeshi wakati mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya NATO wakiendelea kukutana kwa siku ya pili Jumatano. Wakati huo Urusi imejitamba kuvunja ngome za Ukraine mashariki.

https://p.dw.com/p/4NV39
Ukraine | Präsident Selenskyj
Picha: Presidential Office of Ukraine

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Telegram kuwa wanajeshi wa Ukraine walirudi nyuma kufuatia mashambulizi ya Urusi kwenye mkoa wa Luhansk, ingawa haikutoa ufafanuzi na madai hayo hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Ripoti hiyo imesema wakati wa mashambulizi hayo, Waukraine walirudi nyuma umbali wa kilomita 3 kutoka maeneo waliyokuwa awali, na kuongeza kuwa hata msitari wa pili wenye ulinzi mkali ulishindwa kulizuwia jeshi la Urusi.

Soma zaidi: Urusi yashambulia maeneo ya jimbo la Donetsk

Uongozi wa jeshi la Ukraine hata hivyo haukuzungumzia changamoto zozote mkoani Luhansk katika maelezo yake ya asubuhi Jumatano hii, ukisema kwamba vikosi vya Ukraine vilizuwia mashambulizi katika maeneo zaidi ya makaazi 20, ikiwemo Bakhmut naVuhledar, ambao ni mji ulioko umbali wa kilomita 150 kusini-magharibi mwa Bakhmut.

Ukraine-Krieg | Ukrainische Soldaten an der Front bei Bachmut
Wanajeshi wa Ukraine kutoka brigedi ya tatu ya mashambulizi ya kikosi cha operesheni maalum wakiwa eneo la karibu na mji wa Bakhmut, mkoa wa Donetsk, Ukraine, Februari 11, 2023.Picha: Libkos/AP Photo/picture alliance

Zelenskiy: Haraka ni muhimu sana kuokoa maisha

Rais wa Ukraine Volodymyr zelenskiy amesema Urusi ilikuwa inafanya haraka kufanikisha mambo mengi haraka iwezekanavyo kupitia mashambulizi yake ya sasa, kabla ya Ukraine na washirika wake kukusanya tena nguvu.

"Ndiyo maana kasi ni muhimu kwa sasa. Kasi ndiyo kila kitu. Katika kufanya maamuzi. Katika kutekeleza maamuzi. Katika uwasilishaji. Katika mafunzo. Kasi huokoa maisha, kasi hurejesha usalama. Na nawashukuru washirika wetu wanaotambua kwamba kasi ni muhimu," alisema Zelenskiy katika ujumbe wake wa kila usiku kwa njia ya vidio.

Soma zaidi: Ukraine inataka uamuzi wa haraka juu ya ndege za kivita

Ukraine inatumia risasi na makombora kwa kasi kubwa zaidi kuliko mataifa ya magharibi yanavyoweza kuvitengeneza, na inasema inahitaji ndege za kivita na makombora ya masafa marefu kukabiliana na mashambulizi ya Urusi na kurejesha maeneo iliyoyapoteza.

Marekani na jumuiya ya kujihami ya NATO wameahidi kwamba msaada wa magharibi hautasita mbele ya mashambulizi yajayo ya Urusi. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, amesema anatarajia Ukraine kuanzisha mashambulizi yake yenyewe katika msimu wa machipuko.

NATO Treffen Brüssel Lloyd Austin
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, amesema anataraji Ukraine kuanzisha mashambulizi msimu wa machipuko kurejesha maeneo yaliotwaliwa na Urusi.Picha: AP

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema utoaji wa ndege za kivita kwa Ukraine utajadiliwa, lakini siyo suala kuu kwa sasa. Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amesema Uingereza inatoa mafunzo kwa Waukraine kupigana kwa njia ya kimagharibi zaidi, na kutumia risasi kidogo zaidi kuliko ilivyo kwa njia ya kisovieti.

Soma zaidi: NATO yaonya juu ya uhaba wa risasi Ukraine

Urusi ambayo inauita uvamizi wake kuwa operesheni maalumu ya kijeshi yenye lengo la kuondoa vitisho vya kiusalama, imesema NATO imeonyesha uhasama wake kuelekea Urusi kila siku, na ilikuwa inazidi kujihusisha zaidi na zaidi kwenye mzozo nchini Ukraine. Ukraine na washirika wake wanavitaja vitendo vya Urusi kuwa unyakuzi wa ardhi usiyo na msingi.

Chanzo: rtre, aptn.