1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine inataka uamuzi wa haraka juu ya ndege za kivita

14 Februari 2023

Ukraine imesema inatarajia washirika wake wa Magharibi wafikie makubaliano ya kuipatia nchi hiyo silaha za kivita.

https://p.dw.com/p/4NSF6
Ukraine | Sukhoi Su-25 Kampfjet | Tag der Seestreitkräfte
Picha: Yulii Zozulia/Avalon/Photoshot/picture alliance

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrij Melnyk, ametoa wito wa kufikiwa maamuzi ya haraka kuhusu suala la ndege za kivita kupelekwa Ukraine, wakati ambapo mji wa Bakhmut ukikabiliwa na mapigano makali siku chache kabla ya kutimia mwaka mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Akizungumza na kituo cha utangazaji cha Ujerumani, ARD, Melnyk amesema kwamba wataalamu wa Ujerumani wametoa wito wa kupelekwa ndege hizo kwa hiyo ni suala la muda tu.

Ukraine itakabiliwa na changamoto ya kushinda Urusi

Amesema suala hilo linapoendelea kucheleweshwa, ndivyo itakavyokuwa changamoto zaidi kwa Ukraine kuishinda Urusi.

Kwa mujibu wa Melnyk, mbali na kuchelewesha kufikia maamuzi, hakuna marubani wa Ukraine wanaopatiwa mafunzo, wakati ambapo Rais wa Urusi Vladmir Putin, anaweza kuendelea kupeleka vifaru kwenye maeneo ya mapambano.

Ama kwa upande mwingine mji wa Bakhmut umekuwa ukikabiliwa na mashambulizi makali.

Muungano wa Kijeshi wa NATO ukiunga mkono taarifa za maafisa kwenye eneo hilo kwamba Urusi imeanzisha mashambulizi mapya siku chache kabla ya kutimia mwaka mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Russland - Ukraine - Konflikt - Bakhmut
Wanajeshi wakiwa kwenye kifaru kwenye mji wa Bakhmut, Ukraine Picha: Yevhen Titov/REUTERS

Afisa wa jeshi la Ukraine amesema Jumanne kuwa wanajeshi wake kwenye mji huo wa mashariki walikuwa wakikabiliana na mashambulizi mapya ya makombora ya vikosi vya Urusi.

Vikosi vya Ukraine vimezuia mashambulizi ya Urusi kwenye eneo moja la makaazi katika jimbo la Kharkiv, maeneo matano ya makaazi kwenye jimbo la Luhansk na maeneo sita ya makaazi kwenye jimbo la Donetsk, ikiwemo mji wa Bakhmut, katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Gavana wa Donetsk, Pavlo Kyrlenko amesema hakuna hata mita moja ya mraba mjini Bakhmut ambayo iko salama au ambayo haijalengwa kwa mashambulizi ya makombora au ndege zisizo na rubani za adui yake.

Vikosi vya Urusi vinakusudia kuliteka jimbo lote la Luhansk na kuifikia mipaka yake ya kiutawala.

NATO: Ukraine inahitaji silaha zaidi

Huku hayo yakijiri Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kijihami ya NATO, Jens Stoltenberg amesema Ukraine inahitaji kupatiwa silaha zaidi inazohitaji ili kuvishinda vita hivyo.

Akizungumza Jumanne na waandishi habari baada ya kuwasili mjini Brussels kuhudhuria mkutano wa kilele wa siku mbili wa mawaziri wa ulinzi wa NATO, Stoltenberg amesema wameona jinsi Urusi inavyopeleka majeshi zaidi, silaha zaidi, kuimarisha uwezo wake zaidi, akisema huo ni mwanzo mpya wa mashambulizi.

"Hatuoni ishara yoyote kwamba Rais Putin anajiandaa kwa mazungumzo ya amani. Kile tunachokiona ni kinyume chake. Anajiandaa kwa vita na mashambulizi zaidi. Hivyo, ni muhimu kwamba washirika wa NATO watoe msaada zaidi kwa Ukraine," alisisitiza Stoltenberg.

Belgien | Treffen der Nato-Verteidigungsminister in Brüssel
Katibu Mkuu wa NATO, Jens StoltenbergPicha: Johanna Geron/REUTERS

Hata hivyo, Stoltenberg amesema Ukraine inatumia risasi kwa haraka zaidi kuliko wanachama wa NATO wanavyoweza kuzitengeneza. Amesema NATO inatarajia kuongeza silaha zake na risasi, kutokana na vita kupunguza akiba iliyopo.

Mafunzo kwa wanajeshi wa Ukraine

Wakati huo huo, mafunzo kwa wanajeshi wa Ukraine kwa ajili ya matumizi ya vifaru chapa Leopard 2 na vifaru vingine vya kisasa kwa lengo la kuviimarisha vikosi vya Ukraine, yanaendelea kwenye nchi kadhaa za Ulaya, ikiwemo Poland, Uingereza na Ujerumani.

Aidha, ofisi inayoshughulikia haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema siku ya Jumatatu kwamba imerekodi vifo vya raia 7,199 na wengine 11,756 waliojeruhiwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24, 2022.

Vifo vingi vimesababishwa na mashambulizi ya anga na makombora. Hata hivyo, inaaminika kuwa idadi kamili ni kubwa zaidi ya hii.

 

(AFP, DPA, Reuters, DW)