Ukraine yaandaa mkutano wa amani Denmark
24 Juni 2023Wajumbe kwenye mkutano huo wanajadili njia ya kuelekea kwenye amani. Mpaka sasa ni taarifa chache zinazojulikana juu ya mkutano huo. Hata hivyo afisa mmoja wa nchi za Magharibi ambaye hakutaka kutajwa amesema mshauri wa usalama wa Marekani Jake Sullivan anahudhuria.
Ameeleza kuwa mkutano wa Copenhagen unajikita katika kujadili njia za kuleta amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine. Walioalikwa ni pamoja na maafisa wakuu wa usalama kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zinanazoiunga mkono Ukraine.
Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya ameeleza kuwa ndani ya nchi tajiri saba duniani imefanyika kazi ya bidii kubwa kutayarisha mwongozo wa amani. Gazeti la Uingereza la Financial Times lililokuwa la kwanza kuripoti juu ya mkutano huo lilinukuu vyanzo vilivyosema kuwa China, India na Afrika Kusini pia zitashiriki kwenye mkutano wa nchini Denmark.