Afrika Kusini yasifia ujumbe wa kihistoria wa amani Ukraine
19 Juni 2023Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amepongeza hii leo ujumbe wa Afrika wa kuleta amani nchini Ukraine na kuutaja kuwa wa "kihistoria". Ramaphosa ameyasema hayo aliporejea katika ziara yake mjini Kyiv na Saint Petersburg. Rais Ramaphosa amesema: " Nadhani ziara yetu ilikuwa na matokeo chanya. Mafanikio ya kweli yatapimwa kwa lengo kuu la kusitisha vita. Pengine sisi ndio ujumbe pekee uliowashirikisha viongozi hao wawili ndani ya muda mfupi kunako pendekezo la kutaka kusitisha vita hivi.
Wajumbe hao wa ngazi ya juu wa Afrika ambao ni marais wa Afrika Kusini, Zambia, Comoro na waziri mkuu wa Misri, walikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumamosi kabla ya kusafiri kwa ndege kuelekea Urusi kuzungumza na rais Vladimir Putin siku ya Jumapili. Walitoa mapendekezo kadhaa ya kufikia hatimaye makubaliano ya kusitisha vita.
AFP