1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Urusi inadhibiti asiliamia 70 ya Severodonetsk

1 Juni 2022

Ukraine imesema vikosi vya Urusi vinadhibiti takribani asilimia 70 ya mji wa Severodonetsk, wakati ambapo Marekani na Ujerumani zikitangaza kupeleka Ukraine mifumo ya kisasa ya makombora ya kuzuia mashambulizi.

https://p.dw.com/p/4C7sT
Ukraine - Zerstörung in Luhansk
Picha: Serhii Nuzhnenko/REUTERS

Akizungumza siku ya Jumatano, Gavana wa jimbo la Luhansk, Serhiy Gaidai amesema mapigano yanapamba moto, huku Urusi ikijaribu kulidhibiti eneo la mashariki la Luhansk. Kauli hiyo ameitoa kupitia mtandao wa mawasiliano wa Telegram, na kusema kwamba baadhi ya wanajeshi wa Ukraine wamerudi nyuma, baada ya mashambulizi kuongezeka katika mji wa kimkakati wa Severodonetsk.

Mapigano katika mji huo yaliongezeka Mei 30 na 31. Severodonetsk, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Luhansk ndiyo eneo la mwisho katika jimbo hilo ambao unadhibitiwa na vikosi vya jeshi la Ukraine.

Ujerumani kupeleka Ukraine mifumo ya kuzuia mashambulizi

Huku hayo yakijiri, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema nchi yake itapeleka Ukraine mifumo ya kisasa ya roketi kuzuia mashambulizi ya anga, aina ya IRIS-T. Akilihutubia bunge la Ujerumani, Bundestag Jumatano, Scholz amesema Ujerumani iliahidi kuipatia Ukraine mfumo wa rada wenye uwezo wa kufuatilia na kugundua ndege za adui, roketi pamoja na makombora.

''Pia tutapeleka silaha zaidi katika wiki zijazo. Kwa mfano, serikali ya Ujerumani imeamua kwamba tutapeleka mfumo wa IRIS-T, mfumo wa kisasa zaidi wa kujilinda na mashambulizi ya anga. Itaisaidia Ukraine kujilinda na mashambulizi ya anga ya Urusi. Huo pia ni uamuzi wa serikali hii ya shirikisho," alifafanua Scholz.

Generaldebatte der Haushaltswoche im Bundestag
Kansela wa Ujerumani, Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/picture alliance/dpa

Kansela huyo wa Ujerumani ameutangaza mpango huo, muda mfupi baada ya Rais wa Marekani, Joe Biden naye kusema ataipatia Ukraine mifumo ya kisasa ya makombora, wakati ambapo vikosi vya Urusi vinajaribu kuuteka mji muhimu wa mshariki ya Ukraine. Mifumo hiyo ya makombora ni sehemu ya euro milioni 653 za fedha za msaada wa silaha unaotarajiwa kutangazwa baadae leo. Msaada huo wa usalama unajumuisha helikopta, mifumo ya silaha za kuzuia mashambulizi ya vifaru, magari ya kijeshi, mfumo wa rada na magari ya kivita.

Urusi: Mpango wa Marekani unazidisha hatari

Hata hivyo, Urusi imesema Jumatano kuwa mpango wa Marekani kupeleka silaha mpya Ukraine pamoja na mifumo ya kuzuia mashambulizi, unaongeza hatari ya Marekani kujiingiza moja kwa moja kwenye mzozo na Urusi.

Naye kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amewasihi viongozi kuondoa vizuizi vya mauzo ya ngano kutoka Ukraine, akisema kwamba nafaka hiyo haiwezi kutumika kama silaha ya kivita. Akizungumza Jumatano mbele ya maelfu ya waumini katika Uwanja wa Mtakatifu Peter, Vatican, Papa Francis amesema vizuizi hivyo vinapaswa kuondolewa kwa sababu mamilioni ya watu hasa katika nchi masikini zaidi duniani wanategemea ngano kutoka Ukraine.

Schulcamp für intern vertriebene ukrainische Kinder
Watoto wa Ukraine walioathiriwa na vita wakiwa katika kambi moja magharibi mwa nchi hiyoPicha: Emmanuelle Chaze/DW

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF limesema zaidi ya watoto milioni tano wa Ukraine wanategemea msaada wa chakula.

Ndani ya Ukraine kwenyewe, watoto milioni tatu wanahitaji msaada na wengine milioni 2.2 waliokimbia vita Ukraine wanahitaji pia msaada. Kwa mujibu wa UNICEF, watoto wapatao 262 wameuawa tangu vita vilipoanza na mamia ya shule zimeharibiwa.

Ama kwa upande mwingine, kampuni ya nishati ya Denmark Orsted, imesema Urusi inasitisha kupeleka gesi asilia kwenye nchi hiyo ya Scandnavia, baada ya kukataa kulipia gesi kwa sarafu ya Urusi ya Ruble.

(DPA, AP, AFP, Reuters, DW)