Zoezi la kuwahamisha raia kwenye mji wa Mariupol laendelea
6 Mei 2022Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema oparesheni ya tatu ya kuwahamisha raia kutoka mji wa bandari wa Mariupol na katika kiwanda cha chuma cha Azovstal kilichozingirwa inaendelea. Msimamizi wa ofisi ya rais wa Ukraine Andriy Yermak, amesema takriban raia 500 wameokolewa katika operesheni inayoongozwa na Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Shirika la msalaba mwekundu ICRC, katika mji wa Mariupol.
Mji huo ulio kusini mwa Ukraine kwenye bahari ya Azov, ni miongoni mwa miji iliyoharibiwa vibaya kutokana na vita vilivyodumu kwa wiki ya 10 sasa. Eneo la kiwanda cha chuma cha Azovstal ndio la mwisho katika mji huo linaloshikiliwa bado na vikosi vya Ukraine.
Soma:Urusi yazidisha mashambulizi katika mji wa Odessa
Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Ukraine, takriban raia 200 bado wamekwama katika kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol. Mwakilishi wa jeshi la Ukraine amesema Urusi inaendelea na mashambulizi kwenye kiwanda hicho cha chuma cha Azovstal.
Soma:Zelensky: Urusi imeshambulia hospitali na vituo vya matibabu
Wakati huo huo Ujerumani imetangaza kuwa itapeleka silaha zaidi wa ajili ya ulinzi wa Ukraine. Wizara ya ulinzi ya Ujerumani imesema miongoni mwa silaha itakazopeleka nchini Ukraine ni mizinga inayojifyatua yenyewe. Uamuzi wa kupeleka silaha hizo nzito unatokana na mabadiliko ya sera ya Ujerumani baada ya nchi hiyo kulaumiwa kwa kusita kupeleka silaha za aina hiyo nchini Ukraine. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Christine Lambrecht amesema silaha hizo aina ya Howitzer, yaani mizinga inayojifytua yenyewe ndizo hasa ambazo Ukraine inazihitaji kwa ajili ya kujihami dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Jeshi la Urusi lilitangaza siku tatu za kusimamisha mapigano kuanzia Alhamisi na limewataka wapiganaji wa Ukraine waliomo kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal waweke silaha chini. Wakati huo huo msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov ameeleza kuwa nchi za magharibi zinaipatia Ukraine taarifa za kipelelezi wakati wote. Hata hivyo msemaji huyo ameeleza kuwa nchi za magharibi hazitaweza kuyazuia malengo ya majeshi ya Urusi nchini Ukraine.
Soma pia: Mapambano makali yaripotiwa kiwandani Mariupol
Urusi pia imezilaumu nchi za magharibi kwa kuichelewesha kampeni yake ya kijeshi nchini Ukraine na wizara ya ulinzi ya Marekani imekanusha madai kwamba nchi hiyo imekuwa inawapa wanajeshi wa Ukraine habari za kipelelezi juu ya majenerali wa Urusi ili waweze kuwaua.
Vyanzo:RTRE/DPA