Marais wa Ujerumani na Ukraine wasuluhisha mzozo wao
5 Mei 2022Mapigano katika eneo lililozingirwa na majeshi ya Urusi la kiwanda cha chuma katika mji wa Mariupol yamepamba moto huku vikosi vya Urusi vikijaribu kukamilisha zoezi la kuudhibiti mji huo wa bandari ambao ni muhimu kimkakati. Urusi inataka kuunganisha mji huo na Rasi ya Crimea, iliyo chini ya Urusi tangu mwaka 2014. Huku hayo yakitokea, takriban dola bilioni 6.5 zimekusanywa kwenye mkutano wa kimataifa wa wafadhili wa Ukraine uliofanyika mjini Warsaw, Poland. Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki ameyasema hayo leo hii.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kabla ya mkutano huo alizindua jukwaa la kimataifa la wafadhili kwa ajili ya kuisaidia nchi yake kushinda vita vinavyoendeshwa na Urusi na pia kusaidia katika ujenzi mpya wa miundombinu ya Ukraine.
Zelensky akizungumza kwa lugha ya Kiingereza kwenye video iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter alisema ili Ukraine ipate ushindi, michango ni muhimu. Rais Zelensky, mwenye umri wa miaka 44, anahutubia mabunge mbalimbali kote ulimwenguni karibu kila siku, akiomba kuungwa mkono dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini mwake.
Mkutano huo wa leo Alhamisi uliandaliwa kwa pamoja na Poland na Sweden na ulihudhuriwa na mawaziri wakuu na mabalozi wanaowakilisha nchi za Ulaya, pamoja na nchi zingine za mbali zaidi na kampuni za biashara.
Vile vile kwa msaada kutoka kwa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Baraza la Ulaya, Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu. Shirika la Fedha Duniani (IMF) limetabiri kuwa pato jumla la taifa la Ukraine litashuka kwa asilimia 35 katika mwaka huu wa 2022 ikiwa ni matokeo ya uvamizi wa Urusi nchini humo.
Wakati huo huo, ofisi ya Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier mjini Berlin imesema Steinmier amezungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa njia ya simu na wamesuluhisha mzozo kati yao juu ya ziara ya rais wa Ujerumani ya mjini Kiev ambayo ilikataliwa na rais wa Ukraine. Steinmeier alipanga kwenda katika mji huo mkuu wa Ukraine pamoja na viongozi wa Poland, Latvia, Estonia na Lithuania ziara iliyofanyika katikati ya mwezi Aprili, lakini aliambiwa katika kipindi cha muda mfupi kuwa asiende nchini Ukraine.
Uamuzi wa serikali ya Ukraine ulichukuliwa wakati ambapo Steinmeier alikuwa anakosolewa kutokana na uhusiano wake na Urusi wakati akiwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na jinsi alivyoshindwa kuzingatia maonyo kutoka kwa nchi za Mashariki mwa Ulaya ambazo ni majirani wa Ujerumani kuhusu kitisho cha kuvamiwa na Urusi.
Vyanzo:AFP/DPA