1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukimwi bado tishio

Mohammed Khelef1 Desemba 2014

Leo ni siku ya Ukimwi Duniani, ambapo mwaka huu umetajwa kuwa ni mwanzo wa mwisho wa Ukimwi, lakini wanaharakati wanasema bado hiyo haimaanishi kwamba maradhi haya thakili yatamalizika hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/1DxUJ
Wanaharakati wakiwa kwenye maandamano ya kupatikana dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi.
Wanaharakati wakiwa kwenye maandamano ya kupatikana dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi.Picha: AP

Kenya, taifa la nne duniani kwa kuwa na maambukizi mengi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) imeshuhudia kiwango kikubwa cha kupungua kwa maambukizi mapya ndani ya kipindi cha miaka ya hivi karibuni, ingawa hali kwenye mitaa ya mabanda katika mji mkuu Nairobi ni ngumu, hasa kwa wanawake ambao bado wanaishi chini ya kivuli cha ugonjwa huo.

Takribani thuluthi moja ya wakaazi wa Nairobi wanaishi kwenye mtaa wa madongo-poromoka wa Kibera, ambako mtu mmoja katika kila watano anaishi na VVU. Kwenye mtaa huu, wanawake wengi masikini hulazimika kujiingiza kwenye biashara ya ngono ili kujikimu kimaisha, wakiwa hawana muamko wa kujikinga.

"Ukosefu wa pesa ni sababu kubwa kwa wanawake wa Kibera kuambukizwa VVU. Wanawake hawana pesa ya kuwawezesha kuishi, hivyo wanawageukiwa wanaume kuomba msaada, ambao nao kawaida hudai penzi na wanakataa kuvaa mipira ya kiume, na hivyo ndivyo hupata pesa kwa ajili ya chakula na watoto wetu, lazima tukubali na hivyo tunaambukizwa," anasema Caroline Akoth, mjane anayeishi kwenye mtaa huu wa mabanda na ambaye kazi yake ya udobi na kuuza vinywaji inaweza kumpatia dola mbili tu kwa siku.

Msaada wa matibabu

Caroline alianza kupata matibabu miaka mitano iliyopita kwa msaada wa jumuiya moja isiyo ya kiserikali. Miongoni mwa wafanyakazi wa huduma za kijamii kwenye mtaa wa Kibera ni Joyce Waithera Wambui, ambaye anasema huwasaidia wanawake wote wanaoshi kwenye mazingira magumu.

Upimaji Ukimwi nchini Uganda.
Upimaji Ukimwi nchini Uganda.Picha: picture alliance/Yannick Tylle

"Wanawake hawa wanahitaji msaada zaidi. Tunawafunza stadi za maisha, hatua za kujikinga na afya kwa ujumla. Kwa wale amba tayari wameshaambukizwa, tunawagawia mipira ya kinga na kuwaambia namba ya kuishi na kuvidhibiti virusi hivyo."

Kufikia mwaka jana, asilimia sita ya wale wanaoishi na VVU nchini Kenya walikuwa na umri wa kati ya miaka 15 na 49. Mwaka 1996, hali ilikuwa mbaya zaidi, ambapo asilimia 10.8 walikuwa wameambukizwa. Margaret, mwanamke wa miaka 24 ni kahaba kwenye mtaa huo wa mabanda, ambaye amekuwa akiishi na Ukimwi kwa mwaka wa 10 sasa.

"Sikuwa nikijua chochote kuhusu Ukimwi hadi nilipoambukizwa. Mwanzoni niliona aibu na kudhani nimeiletea laana familia yangu. Sikuthubutu hata kuwaangalia watu kwani nilidhani wangelijuwa kuwa nimeambukizwa VVU," anasema Margaret.

Mwanzoni mwa ugonjwa wake, Margaret akageukia pombe kulainisha machungu yake, lakini binti yake akampa moyo wa kuendelea na maisha. Hata hivyo, anaendelea kufanya kazi yake ya ukahaba, kwani anasema hana ujuzi mwengine wa kumuwezesha kuishi.

Vidonge na kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi, VVU.
Vidonge na kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi, VVU.Picha: I.Kasamani/AFP/GettyImages

"Hali niliyonayo inanitia majonzi. Sitaki niwe hivi. Ninataka familia ambapo nitaitwa mke na mama, lakini kamwe sitaweza kulipata hilo. Sitaweza kujihisi chochote na yeyote kwa sababu ya Ukimwi," anasema mwanamke huyo.

Hali halisi kwa sasa

Kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa inayopigania kukomesha umasikini na maradhi yanayozuilika barani Afrika, ONE Campaign, idadi ya walioambukizwa mwaka jana ilikuwa ndogo kuliko ya wale waliojiunga na huduma ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka jana, watu milioni 35 duniani walikuwa wanaishi na ugonjwa huo, huku milioni 2.1 wakiwa wagonjwa wapya na milioni 1.5 wakifariki dunia kutoka na maradhi yasababishwayo na Ukimwi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reueters/AFP
Mhariri: Josephat Charo