Ukatili dhidi ya watoto kwenye vita umeongezeka sana 2023
12 Juni 2024Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaeleza ukatili dhidi ya watoto katika maeneo yaliokumbwa na migogoro kwa mwaka 2023 umefikia viwango vya juu kwa idadi isiyo ya kawaida ya mauaji na majeruhi kuanzia Israel na maeneo ya Palestina hadi Sudan, Myanmar na Ukraine.
Ripoti ya kila mwaka ya Watoto walio katika Migogoro ya Kivita, inaonesha kunaongezeko kubwa la asilimia 21 la vurugu zenye kusababisha madhila ya watoto wa chini ya umri wa miaka 18, ikitolea mfano wa Kongo, Burkina Faso, Somalia na Syria.
Kwa mara ya kwanza, ripoti hiyo inaiyaweka majeshi ya Israel kwenye yake orodha mbaya ya nchi zinazokiuka haki za watoto kwa mauaji na kulemaza watoto na kushambulia shule na hospitali. Kadhalika kwa mara ya kwanza limeorodheshwa kundi la Hamas kwa kuua, kuwajeruhi na kuwateka nyara watoto.
Israel na wanamgambo wa Hamas wameingia katika rekodi mbaya
Shambulio la kushtukiza la Hamas Oktoba 7 kusini mwa Israel na kitendo cha Israel katika ulipizaji kisasi mkubwa wa kijeshi huko Gaza umesababisha ongezeko la asilimia 155 la ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto, hasa kutokana na matumizi ya silaha za miripuko katika maeneo yenye watu wengi huko Gaza.
Umoja wa Mataifa umeviweka vikosi vya jeshi la Urusi na makundi washirika wake yenye kujihami kwa silaha kwenye orodha yake mbaya kwa mwaka wa pili juu ya mauaji yao na kulemaza watoto na kushambulia shule na hospitali nchini Ukraine.
Ripoti iliendelea kusema kwa mwaka huo uliopita Umoja wa Mataifa ulithibitisha kuuwawa kwa watoto 80 wa Ukraine na kulemazwa wengine 419 kulikofanywa na vikosi vya Urusi na washirika wake, wengi kutokana na silaha za miripuko.
Ongezeko la asilimia 480 la ukiukwaji dhidi ya watoto
Sudan, ambako kumekuwa na vita kati ya majenerali wapinzani wanaowania mamlaka inayoendelea tangu 2023, kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la asilimia 480 la hali ya ukiukwaji mbaya dhidi ya watoto.
Soma zaidi:Unicef : Watoto milioni 400 wanakabiliwa na adhabu za vipigo
Katika ripoti hiyo mpya Umoja wa Mataifa umeyataja mataifa kama Afghanistan, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika Kati, Colombia, Kongo, Iraq, Mali, Msumbiji, Nigeria, Ufilipino, Somalia, Sudan Kusini, Syria, Ukraine na Yemen kama maeneo ambayo usalama watoto umeendelea kudidimia zaidi.
Chanzo: AP