Ujumbe wa UN waelezea wasiwasi wake kuhusu mivutano Libya
27 Agosti 2024Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoisimamia Libya, UNSMIL, umetoa taarifa jana usiku ukieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na kuzorota kwa hali nchini Libya, kutokana na hatua za kufanyika maamuzi ya upande mmoja. Wasiwasi huo umetokana na mvutano kuhusu suala la usimamizi wa benki kuu ya Libya ambao umeibua mashaka juu ya uwezekano wa kutumiwa vibaya kwa vyanzo vya mapato ya fedha vya nchi hiyo.
Soma taarifa hii: Libya yakabiliwa na kitisho cha kuporomoka kwa uchumi
Taarifa ya UNSMIL pia imesema,ujumbe huo umeitisha mkutano kuzikutanisha pande zote husika katika suala la mgogoro unaohusu benki kuu ya Libya ili kufikiwa msimamo wa pamoja utakaozingatia makukubaliano ya kisiasa,sheria zilizopo na misingi ya uhuru wa benki hiyo kuu ya Libya. Serikali yenye makao yake Mashariki mwa Libya siku ya Jumatatu ilitowa agizo la kutaka kufungwa kwa vinu vyote vya mafuta katika eneo hilo,ambavyo kimsingi vinategemewa kwa takribana uzalishaji wa nchi nzima. Hata hivyo hakujakuwa na uthibitisho wowote kuhusu suala hilo kutoka upande wa serikali inayotambuliwa kimataifa ya mjini Tripoli.