Ujerumani yatanua ukaguzi mipakani kudhibiti wahamiaji
16 Septemba 2024Ujerumani ilitangaza hatua hiyo ya kutanuliwa ukaguzi katika mipaka yake kufuatia misururu ya mashambulizi ya itikadi kali, yanayodaiwa kufanywa na wageni, yaliyoongeza hofu nchini humo na kuongeza umaarufu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, kinachopinga wageni cha AFD. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser awali alisema hatua hiyo inayopangwa kufanyika kwa miezi sita, inanuia kudhibiti uhamiaji holela, kuzuia wahalifu na pia kuwatambua mapema watu walio na itikadi kali.
Scholz aitembelea Solingen baada ya shambulizi la kisu
Hata hivyo Poland na Austria zimeelezea wasiwasi wao juu ya ukaguzi huo, na Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imeonya kuwa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zinatakiwa kuweka hatua kama hizo katika mazingira ya kipekee. Kulingana na Umoja huo, wanachama wanaruhusiwa kwa muda kuweka ukaguzi wa mipaka kufuatia kitisho cha usalama wa ndani. Ukaguzi huo sasa utafanyika katika mipaka ya Ujerumani na Ufaransa, Luxembourg, Uholanzi, Ubelgiji na Denmark. Faeser amesema kwa muda huu wa miezi sita, wasafiri mara zote ni lazima wabebe vitambulisho vyao.
Ujerumani kuongeza kasi ya kuwarudisha wahamiaji makwao
Ujerumani inapakana na mataifa tisa ya Ulaya yaliyosehemu ya Schengen, ambayo inaruhusu usafirishaji huru wa watu na bidhaa bila kuhitaji visa. Ukaguzi wa mipaka katika mataifa ya Poland, Jamhuri ya Czech, Austria na Uswisi tayari ulikuwa unafanyika kabla ya hatua hiyo mpya kutangazwa.
Mashambulizi ya mara kwa mara yazidhisha hofu Ujerumani
Mwezi uliopita shambulizi la kisu linalodaiwa kufanyawa na muomba hifadhi kutoka Syria mjini Solingen lilisababisha mauji ya watu watatu. Mshukiwa alidai kushawishika kutoka kwa kundi la Dola la Kiislamu. Mwezi Juni hsambulizi lengine la kisu lililodaiwa kufanywa na raia wa Afghanistan lilisababisha mauaji ya afisa mmoja wa polisi na kuwajeruhi watu wengine wanne.
Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis amesema kwa Ujerumani kudhibiti mipaka yake kunamanisha itatupa mzigo kwa mataifa mengine, huku Waziri wa ndani wa Austria Gerhard Karner akisema nchi yake haitokubali waliokataliwa Ujerumani. Nae Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk ameikosoa Ujerumani kwa kuchukua hatua hiyo ya kutanua ukaguzi katika mipaka yake.
Mshukiwa wa shambulio la Solingen kufikishwa mahakani Karlsruhe
Warsaw pia imekuwa ikihangaika na suala la uhamiaji na kuishutumu Moscow kwa kuwaingiza watu kiharamu Ulaya kutoka bara la Afrika na mashariki ya Kati kwa kuwatuma kupitia Belarus hadi mpakani mwa Poland. Huku uchaguzi Mkuu ukitarajiwa kufanyika mwaka ujao serikali ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz imekuwa chini ya shinikizo kali la kisiasa kusimamia misimamo yake juu ya suala la uhamiaji na waomba hifadhi.
Vyanzo: afp/ap