Baada ya Flick, ni Nagelsmann ama Klopp?
11 Septemba 2023Shirikisho hilo limeona haliwezi kuendelea na Hansi Flick wakati taifa hilo likijiandaa kuwa mwenyeji wa michuano ya Euro mwezi Juni mwakani.
Kipigo hicho cha tatu mfululizo kimeonyesha dhahiri uwezo wa Flick, lakini aliendelea kusalia na kikosi hicho kutokana na mechi kati yao na Ufaransa inayochezwa Jumanne hii. Licha ya hayo, DFB haikuwa tayari kubeba aibu nyingine na kuamua kuachana naye.
Rais wa DFB Bernd Neuendorf amesema "Tumekubaliana kwamba timu ya taifa ya soka ya wakubwa inahitaji mwamko mpya baada ya matokeo mabovu yaliyopita. Tunahitaji ujasiri na hasa kwa kuangazia michuano ijayo ya Ulaya inayofanyika hapa. Kwangu mimi ni uamuzi mgumu sana kuwahi kuufanya nikiwa na wadhifa huu, na hasa kwa kuzingatia ninamthamini sana Hansi Flick na wasaidizi wake. "
Flick aliisaidia Ujerumani kushinda Kombe la Dunia mwaka 2014 akiwa kocha msaidizi na aliyeshinda michezo minane ya awali baada ya tu ya kupewa kikosi cha Ujerumani mwaka 2021.
Kwa sasa shirikisho hilo la DFB linasaka kwa udi na uvumba kocha mpya, taarifa yake ilisema na kocha wa zamani wa Bayern Munich Julian Nagelsmann ndiye anayepigiwa upatu zaidi pamoja na kocha wa Liverpool, Jürgen Klopp.