Ujerumani yapinga pendekezo la ukomo wa wakimbizi
26 Septemba 2023Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Faeser amesema pendekezo hilo haliwezi kuzingatiwa kwasababu Ujerumani inafanya kazi chini ya "sheria za Umoja wa Ulaya, sheria za kimataifa na hivyo hawawezi kupunguza haki ya mtu binafsi katika suala la hifadhi pekee."
Kuhusu wakimbizi wa Ukraine: Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani aunga mkono ulinzi kwa wakimbizi wa Ukraine
Markus Söder ambaye ni kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Bavaria cha Christian Social Union CSU, alitoa pendekezo kwa Kansela Olaf Scholz kulifanya suala la wahamiaji kuwa kipaumbele cha juu.
Alisema Kansela Scholz, anapaswa kulifanyia kazi suala hilo baada ya kuwa kimya kwa wiki kadhaa na kuonyesha uongozi wake ikiwemo pia kuwashawishi washirika katika mmungano wa serikali yake.
Lakini kwa mujibu wa waziri Faecer, kitu pekee kinachoweza kusaidia ni "suluhisho la Ulaya."
Soma pia: Steinmeier: Ujerumani imefikia ukomo wa kupokea wahamiaji
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock siku ya Jumatatu naye alisisitiza wito huo wa suluhisho la pamoja la Ulaya katika sera ya wakimbizi.
Alisema kwamba hali imekuwa ya wasiwasi katika manispaa za Ujerumani na kwamba ndio maana wanafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kwamba Ulaya inafikia "kanuni za pamoja za sera za hifadhi na wakimbizi".
Ujerumani yahemewa na wimbi la wakimbizi?
Manispaa za Ujerumani hivi karibuni zilielezea wasiwasi wao kuhusu msongamano wa watu.
Mwishoni mwa mwezi Agosti, ofisi ya shirikisho ya uhamiaji na wakimbizi ilisajili zaidi ya maombi 204,000 ya awali ya waomba hifadhi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 77 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Hayo yakijiri waziri wa mambo ya nje wa Poland Zbigniew Rau ameishutumu Ujerumani kwa kujaribu kuingilia mambo yake ya ndani baada ya Kansela Scholz kusema Warsaw inahitaji kutoa ufafanuzi wa madai kwamba balozi za Poland za afrika na Asia ziliuza vibali vya muda vya kufanya kazi kwa wahamiaji kwa maelfu ya dola kila mmoja.
Scholz ambaye serikali yake iko chini ya shinikizo ili kudhibiti wahamiaji nchini Ujerumani, aliitaka jirani yake Poland kutoa ufafanuzi wa nini haswa kimetokea.
"Kashfa ya visa inayotokea Poland kwa hivi sasa inahitaji maelezo. Sitaki kuona Poland inaruhusu watu kuingia kwa urahisi kisha baadae tunajadili kuhusu sera za kuomba hifadhi. Wale wanaowasili Poland lazima wasajiliwe na wapitie mchakato wa kuomba hifadhi huko na wasifanye tatizo kuwa kubwa kwa kutoa tu visa kwa ajili ya fedha."
Lakini kauli ya Scholz ilionekana kuikasirisha Poland iliyosema kwamba inakiuka "kanuni za usawa wa uhuru wa nchi".Chama tawala cha mrengo wa kulia cha sheria na haki, kinakabiliwa na maswali kuhusu shutuma hizokelekea uchaguzi wa kitaifa wa Oktoba 25 ambapo kinatafuta muhula wa tatu madarakani.