Ujerumani yajitetea katika mahakama ya ICJ
9 Aprili 2024Wakili wa Ujerumani katika kesi hiyo inayosikilizwa katika mahakama ya ICJ Tania von Uslar-Gleichen, ameiambia mahakama hiyo kwamba historia ya nchi hiyo ndiyo sababu kuu ya kwanini usalama wa Israel unazingatiwa zaidi katika sera yake ya mambo ya nje.
Uslar-Gleichen, amesema kuwa nia ya msaada wa Ujerumani kwa Israel unaojumuisha silaha na vifaa vingine vya kijeshi,imetafsiriwa kimakosa na Nicaragua.
Ujerumani ina jukumu la kuikumbusha Israel kuhusu sheria ya kimataifa ya kibinadamu
Uslar-Gleichen amesema katika hali ambayo Israel inakabiliwa na mashambulizi yanayoendelea ya wanamgambo wa Hamas, ni jukumu la Ujerumani kuikumbusha kwamba hata inapotumia haki yake ya kujilinda, sheria ya kimataifa ya kibinadamu bado inatumika .
Soma pia: Nicaragua yaiomba Mahakama ya Haki ya Kimataifa kuiagiza Ujerumani kuacha kuiuzia silaha Israel
Ujerumani imeipinga vikali kesi iliyowasilishwa mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa ya haki na Nicaragua, inayoituhumu kuisadia Israel kukiuka mikataba ya haki za binadamu ya kimataifa, kwa kuipatia nchi hiyo silaha na usaidizi wa aina nyingine katika vita vyake vya Gaza.
Jukumu la mataifa yalio chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari
Ujerumani na Israel ni nchi mbili kati ya zaidi ya 150 zinazoshiriki katika mkataba huo, pamoja na Nicaragua.
Hii inamaanisha kuwa kila taifa lililotia saini mkataba huo, lina jukumu la kisheria la kuzingatia masharti yake na kuwa na haki ya kulishtaki taifa lingine rasmi kwa ukiukaji wake.
Madai ya Nicaragua dhidi ya Ujerumani
Mnamo Machi 1, Nicaragua iliwasilisha kesi dhidi ya Ujerumani katika mahakama ya ICJ inayodai kuwa Ujerumani kwa msaada wake kwa Israel ikiwa ni pamoja na usambazaji wa silaha imeshindwa kutimiza majukumu yake ya kuzuia madai ya mauaji ya kimbari yaliofanyika na yanayofanyika dhidi ya raia wa Palestina na hivyo basi kuchangia kufanyika kwa mauaji hayo kwa kukiuka mkataba huo na vipengele vyengine vya sheria ya kimataifa.
Soma pia:Mahakama ya Haki yaanza kusikiliza kesi dhidi ya Ujerumani
Nicaragua imeitaka ICJ, kuweka hatua za dharura kuizuia Ujerumani kutoa silaha zaidi kwa Israel pamoja na msaada mwingine.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamevishtumu vikosi vya Israel kwa mauaji ya kiholela dhidi ya raia. Mataifa washirika wa Israel kama Marekani pia wametaja idadi ya vifo vya raia kuwa juu.