1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 80 ya machafuko dhidi ya Wayahudi

9 Novemba 2018

Ujerumani inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 tangu kuzuka kwa ghasia kubwa zilizofanywa na wafuasi wa Nazi dhidi ya Wayahudi. Angalau Wayahudi 100 waliuawa katika machafuko hayo yaliyoripuka Novemba 9 hadi 13, 1938. 

https://p.dw.com/p/37wDT
Novemberpogrome 1938 Zerstörte jüdische Geschäfte in Magdeburg
Picha: Bundesarchiv, Bild 146-1970-083-42/CC-BY-SA

Rais wa Shirikisho la Ujerumani Frank Walters-Steinmeier na Kansela Angela Merkel wataungana pamoja wajumbe wa Baraza kuu la Wayahudi nchini Ujerumani hii leo kwenye kumbukumbu ya miaka 80 tangu kuzuka kwa ghasia kubwa zilizofanywa na wafuasi wa Nazi dhidi ya Wayahudi. 

Mamia ya masinagogi na biashara zilizokuwa zikimilikiwa na Wayahudi ziliharibiwa na kuchomwa moto, huku mamia kwa maelfu ya Wayahudi wakidhalilishwa hadharani na kufukuzwa nchi. Angalau Wayahudi 100 waliuawa katika machafuko hayo yaliyoripuka Novemba 9 hadi 13, 1938.

Kuzinduliwa kwa kampeni hiyo ya uhalifu kulikofanywa na utawala wa Kinazi dhidi ya Wayahudi walioishi Ujerumani, baadaye kulitambulika kama kama usiku wa Kioo Kilichovunjika, kwa kuwa mitaa yote ilifunikwa na vifusi vya vioo vya madirisha ya mali zilizomilikiwa na Wayahudi, ambayo yaliharibiwa vibaya. 

Deutschland Stolpersteine für die Familie Frankenthal Leipzig
Ni kawaida kuadhimisha kumbukumbu ya siku hii katika maeneo mbalimbali ya UjerumaniPicha: DW/K. Brady

Wakati Ujerumani ikiadhimisha siku hii, mwandishi wa nyaraka nyingi zilizohusu enzi ya utawala wa Kinazi, Wolfgang Benz amesema matukio kama yaliyotokea katika mji wa Chemnitz Agosti 26 mwaka huu yanadhihirisha kwa kiasi gani ni rahisi kwa machafuko kama hayo ya mwaka 1938 kuweza kuibuka tena.

Alisema alipozungumza na shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba kimsingi maandamano hayo ya Chemnitz hayakuwalenga Wayahudi pekee, lakini yalionesha ni rahisi kiasi gani machafuko kama yale ya 1938 yanaweza kuibuka tena. 

Rais wa Baraza la Wayahudi Josef Schuster pamoja na Kansela Merkel wanatarajiwa kutoa hotuba katika sinagogi lililopo kwenye mtaa wa Ryke mjini Berlin, ambazo zitarushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha umma. Wageni mbalimbali maarufu kutoka kada za kisiasa, sayansi, viwanda, kanisa na tamaduni, pia watahudhuria.

Filmausschnitt Brennende Neue Synagoge in Breslau
Moja ya masinagogi yaliyocomwa moto kwenye machafuko hayo.Picha: Aureliusz M. Pedziwol

Sinagogi hilo lenye uwezo wa kuchukua waumini 2,000, ndio kubwa zaidi nchini hapa na moja ya sinagogi kubwa barani Ulaya, baada ya sinagogi lililoko katikati ya mji wa Budapest.

Sinagogi hilo pia lilichomwa moto wakati wa machafuko hayo, lakini kamanda wa polisi wa wilaya aliagiza moto huo kuzimwa mara moja, kwa kuwa ulitishia kusambaa hadi kwenye majengo yaliyokaribiana na sinagogi hilo. 

Inakadiriwa idadi ya waliokufa ilikuwa ilipindukia 1,000. Masinagogi 1,400 pamoja na vyumba vya ibada, na biashara 7,500 za Wayahudi ziliharibiwa kabisa. Takriban watu 300,000 waliotambuliwa kama Wayahudi, wengi miongoni mwao wanaume walichukuliwa na kupelekwa kwenye kambi za mateso baada ya usiku huo.

Serikali ya Ujerumani imezuia maandamano yaliyopangwa kufanywa na wanaharakati wa mrengo mkali wa kulia katika kituo kikuu cha treni hii leo, hatua iliyokaribishwa na rais wa baraza hilo la Wayahudi, Schuster. 

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/DW

Mhariri: Mohammed Khelef