Ujerumani yaadhimisha waliopinga Unazi
19 Julai 2019Wapinzani hao wa unazi wanachukuliwa kama nguzo ya demokrasia ya sasa ya Ujerumani, wakati ambapo kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusiana na kuibuka upya kwa siasa za mrengo wa kulia.
Kansela Angela Merkel ambaye atazungumza Jumamosi katika hafla ya kila mwaka ya kula kiapo kwa wanajeshi 400 kabla kutoa hotuba katika hafla hiyo, alitoa heshima zake kwa Kanali Claus von Stauffenberg na alioshirikiana nao katika kupanga jaribio hilo la kumuua Hitler, kuelekea maadhimisho hayo. Merkel alielezea umuhimu wa watu hao kwa Ujerumani ya sasa.
Kansela huyo alisema "pale tutakapoelewa historia yetu ndipo tutakapoweza kujenga mustakabali mwema."
Wengi walikuwa wanawachukulia waliojaribu kumuua Hitler kama wasaliti
Von Stauffenberg alijaribu kumuua Hitler kwa bomu lililokuwa kwenye mkoba mnamo Julai 20 1944 wakati wa mkutano katika makao yake makuu.
Hitler aliepuka nguvu ya mripuko wa bomu hilo baada ya mtu mmoja kuusogeza mkoba huo kando na meza ya karibu iliyosababisha nguvu ya mripuko huo kuelekea upande mwengine. Mpango huo ulitibuka baada ya habari kuenea kwamba Hitler ameponea shambulizi hilo. Von Stauffenberg na wenzake waliokuwa wamepanga shambulizi hilo waliuwawa masaa machache baadae.
Kisa hicho lakini hakikuwaingia wengi akilini baada ya Vita vya Pili vya Dunia kwa kuwa wengi walikuwa bado wanawachukulia hao waliofanya mpango huo wa kumuua Hitler kama wasaliti, kama walivyosema Wanazi baada ya jaribio hilo la mauaji.
Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho ya Upinzani Ujerumani Johannes Tuchel anasema upinzani huo dhidi ya Wanazi ulikuja kukubaliwa miongo kadhaa baadae. Ni mwaka 2004 ndio uchunguzi uluionyesha kuwa kiasi kikubwa cha Wajerumani wanaamini kwamba upinzani dhidi ya Wanazi ni muhimu kwa utamaduni wa kisiasa wa nchi hiyo.
Kuna wasiwasi mkubwa wa kuzuka na kuongezeka kwa siasa za mrengo wa kulia Ujerumani
Tuchel anasema von Stauffenberg awali alikuwa anaunga mkono sera za Wanazi ila alibadilika baada ya Hitler kuuvamia Umoja wa Sovieti mwaka 1941.
Maadhimisho ya mwaka huu yanakuja wakati ambapo kuna wasiwasi mkubwa kuhusiana na kuongezeka kwa watu wanaounga mkono siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani. Haya yanakuja wiki chache baada ya kuuwawa kwa afisa kutoka chama cha Kansela Merkel aliyekuwa anaunga mkono sera yake ya kuwakaribisha wahamiaji.
Mfuasi mmoja wa siasa kali za mrengo wa kulia ambaye aliwahi kufunguliwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya wahamiaji, amekamatwa kama mtu anayeshukiwa kuhusika na mauaji hayo.