Steinmeier ajadiliana na raia wa Chemnitz
2 Novemba 2018Akiwa katika jiji hilo ambalo sasa linahusishwa na itikadi kali za mrengo wa kulia, ujumbe wake ukiwa, tunahitaji kuzungumza.
Picha na vidio zilionekana kote duniani, mbele ya sanamu ya Karl Marx au Nishel kama wenyeji wanavyoiita - ndicho kilikuwa kitovu cha machafuko ya wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia ambazo wengi walifikiri zilitoweka kitambo kutoka kwenye mitaa ya Ujerumani.
Miezi miwili baadae, mambo yametulia. Ishara za wazi za maandamano hayo yaliyoishangaza Ujerumani ni mabango mawili ya kupinga siasa hizo za mrengo wa kulia. Mabango hayo yameandikwa "Chemnitz si kijivu wala zambarau," yakiashiria rangi ambazo kitamaduni zilihusishwa na mrengo wa kulia.
Steinmeier ameitembelea Chemnitz kawa mara ya kwanza kama Rais
Kufuatia mauaji ya Daniel H. mwezi Agosti maelfu ya waandamanaji waliingia mitaani na kuandamana. Raia mmoja wa Syria na mwenzake wa Iraq wanadaiwa kumuua kwa kumdunga kisu mtu huyo aliyekuwa na umri wa miaka 35 baada ya kutokea mzozo. Maandamano hayo ghafla yaligeuka na kuwa machafuko ya ubaguzi wa rangi yaliyohudhuriwa na watu wanaounga mkono unazi. Baadhi ya waandamanaji walilaumiwa kwa kuwavamia watu walioamini kwamba ni wahamiaji huku wengine wakionekana kupiga saluti ya kinazi ambayo ni marufuku Ujerumani.
Katika juhudi za kuleta maelewano kati ya raia, Rais wa Ujerumani Frank walter Steinmeier ameitembelea Chemnitz kwa mara ya kwanza kama rais ambako amekutana na kundi la raia. Kwa masaa mawili na nusu, raia 13 wa Chemnitz walielezea wasiwasi na maoni yao kwa rais huyo wa Ujerumani pamoja na meya wa Chemnitz Barbara Ludwig. Lakini mazungumzo hayakuwa shwari tu hasa lilipokuja swala la jinsi Ujerumani ilivyoshughulikia mzozo wa uhamiaji mwaka 2015.
Chama cha CDU kimeanza kupoteza uungwaji mkono jimbo la Saxony
Waandamanaji hawakuonekana katika mitaa ya Chemnitz mchana wa Alhamis ingawa mambo yanatarajiwa kuwa tofauti Novemba 16 Kansela Angela Merkel atakapozuru mji huo huo. Maelfu ya waandamanaji wa siasa za mrengo wa kulia wanatarajiwa kuandamana.
Chama cha Kihafidhina cha CDU chake Angela Merkel kimeanza kupoteza uungwaji mkono katika jimbo la Saxony - uliko mji wa Chemnitz - katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kuibuka kwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD. Katika uchaguzi mkuu wa Septemba mwaka jana, AfD kilishinda kwa asilimia 27 katika jimbo la Saxony.
Lakini licha ya hisia kali kutolewa na waliohudhuria mazungumzo hayo na Steinmeier hapo Alhamis, wote walikubaliana angalau kitu kimoja, kwamba mazungumzo ndio mwanzo wa kuyaponya majeraha ya machafuko ya mwezi Agosti.
Mwandishi: Kate Brady
Tafsiri: Jacob Safari
Mhariri: Iddi Ssessanga