1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kurudisha mafuvu ya vichwa ya Afrika Mashariki

Sylvia Mwehozi
19 Januari 2023

Mamlaka katika Makumbusho ya mjini Berlin Ujerumani imesema kuwa iko tayari kurejesha mamia ya mafuvu ya binadamu kutoka makoloni yake ya zamani ya Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4MRQo
No Flash Übergabe von Schädeln der Ovaherero und Nama in Berlin
Picha: dapd

Wakati wa utafiti wao katika Makumbusho ya historia ya zamani, wanasayansi waliyachunguza jumla ya mafuvu 1,135. Kati yake mafuvu 904 yanaweza kuwa yalitokea Rwanda, 202 kutoka Tanzania na 22 ni ya Kenya. Utafiti zaidi wa mafuvu mengine 7 juu ya asili yake haukuwezekana. Makoloni ya iliyokuwa Ujerumani ya Afrika Mashariki wakati huo yalijumisha nchi ambazo sasa ni Burundi, Rwanda, baadhi ya maeneo ya Tanzania na sehemu kidogo ya Msumbiji. Kenya ilikuwa koloni la Uingereza.

Rais wa wakfu wa urithi wa kitamaduni wa Prussia, Hermann Parzinger, mamlaka inayosimamia makumbusho nyingi za mjini Berlin ikiwemo makumbusho ya historia ya zamani, amesema "lengo la wazi la utafiti wa asili juu ya mabaki ya binadamu ni kuyarejesha kwa nchi husika".

Außenministerin Baerbock besucht Nigeria
Shaba za Benin zilizoporwa na UjerumaniPicha: Annette Riedl/dpa/picture alliance

Ameongeza kuwa wako tayari kurudisha haraka mafuvu hayo na kinachosubiriwa sasa ni ishara tu kutoka nchi za asili. Mafuvu hayo mengi yametoka kwenye maeneo ya maziko haswa makaburi lakini baadhi yanatoka kwenye maeneo ya kunyongea watu na katika hali nyingine pia yalipatikana kwenye maeneo ya kunyonga watu ya Wajerumani.

Mabaki hayo ya binadamu yaliyofanyiwa utafiti yanatoka kwenye mkusanyiko wa anthropolojia ya mafuvu yapatayo 7,700 ambayo mamlaka ya Makumbusho ya Berlin iliyachukua kutoka hospitali ya Charite ya Berlin mwaka 2011. Kulingana na mamlaka ya makumbusho, ukubwa wa mkusanyiko na utofauti wa asili ya kijiografia, ulichangia mafuvu yote kushindwa kufanyiwa utafiti.

Mabaki ya binadamu kutoka Afrika Mashariki, ambayo wakati huo yalikuwa yameondolewa, yalikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani, yalichunguzwa kwanza katika mradi wa majaribio. Ili kufafanua asili halisi ya mafuvu hayo ambayo hayakuwa na nyaraka zilizohifadhiwa, kulihitajika kazi kubwa ya kuhifadhi kumbukumbu, ikiwemo utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Rwanda.

Katika miaka ya hivi karibuni, wakfu wa urithi wa kitamaduni wa Prussia umefanya jitihada za kurejesha mabaki kadhaa ya binadamu na kazi za sanaa ambazo ziliibwa na wajerumani na baadhi ya nchi za kikoloni za Ulaya katika kipindi cha nyuma na kuishia katika makumbusho ya Berlin. Miongoni mwa kazi mashuhuri za sanaa ni mamia ya kile kinachoitwa Shaba za Benin ambazo Ujeruamni ilianza kuzirejesha mwishoni mwa mwaka jana nchini Nigeria kufuatia makubaliano baina ya Berlin na Abuja.