1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani inaweza kufanya vyema EURO 2024

9 Agosti 2023

Timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani ina uwezo wa kupata matokeo katika mashindano ya kuwania kombe la EURO 2024 licha ya kuwa katika hali ambayo si nzuri kwa sasa.

https://p.dw.com/p/4UxCe
Frankfurt | Vorstellung Rudi Völler als neuer Sportdirektor der A-Nationalmannschaft
Picha: Christopher Neundorf/Kirchner-Me/picture alliance

Makamu wa rais wa shirikisho la soka la Ujerumani, Hans-Joachim Watzke, amesema timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani bado ina muda wa kujiimarisha na kujinasua kutoka kwa matokeo mabaya ya mechi za kimataifa ya miaka michache iliyopita na kupata mafanikio katika mashindano ya kombe la EURO 2024 katika udongo wa nyumbani mwakani. Hata hivyo Watzke amesema Wajerumani wanatakiwa watambue upya nguvu zao.

Wajerumani, ambao ni mabingwa mara nne wa kombe la dunia la kandanda na mabingwa mara tatu wa kombe la EURO, wamewahi kupigwa kumbo na kutolewa nje katika mashindano mawili ya kombe la dunia yaliyopita nchini Urusi 2018 na Qatar 2022.

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Hansi Flick, alichukua mikoba baada ya timu kutolewa nje ya mashindano ya EURO 2021 na licha ya timu yake kuanza vyema kwa kupata ushindi, imekuwa ikipata matokeo ya kuvunja moyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

"Bado tuna fursa ya kucheza vyema katika mashindano ya kombe la EURO," alisema Watzke, ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya ligi ya Ujerumani, DFL, na Afisa Mkuu mtendaji wa klabu ya Borussia Dortmund. "Lakini hatimaye tunatakiwa tuanze kujionyesha tofauti," aliliambia jarida la michezo la Bild. "Kila mmoja anafahamu kwamba muda wa majaribio umefika mwisho."

Deutschland Pressekonferenz Kader WM 2022 Hansi Flick
Hansi Flick, kocha wa timu ya taifa ya UjerumaniPicha: Hasan Bratic/DeFodi Images/picture alliance

Ujerumani wameshinda mechi moja tu kati ya tano za mwisho walizocheza tangu kutolewa kwa mshangao katika kombe la dunia Qatar Desemba mwaka uliopita. Pia wameshinda mechi tatu tu kati ya kumi na moja walizocheza mara ya mwisho.

Huku mashabiki wa Ujerumani wakiwazomea na kuwabeza katika mechi za hivi majuzi, Flick anakabiliwa na shinikizo na mustakhbali wake unategemea jinsi watakavyopata matokeo katika mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya Japan Septemba 9 na Ufaransa Septemba 12. Ufaransa walikamilisha mashindano ya kombe la dunia Qatar 202 waliposhindwa na Argentina.

"Pia tunatakiwa tujaribu na tutegemee maadili yetu, hata kama hili linaonekana kuwa jambo dogo lisilo na umuhimu mkubwa," alisema Watzke.

Soma zaidi: Ujerumani imejiandaa vipi kwa EURO 2024

Kwa miongo kadhaa Ujerumani walisifika sana kwa hulka yao ya kutokata tamaa uwanjani na jinsi walivyojilinda kwa nguvu na bidii. Katika miaka 10 iliyopita Ujerumani imekuwa timu yenye mbinu na ujuzi zaidi na yenye fikra za kushambulia katika mchezo wao lakini licha ya kushinda kombe la dunia 2014 hawajafanikiwa kuweka alama katika mashindano ya kimataifa tangu wakati huo.

Safu yao ya ulinzi pia imekuwa ikikabiliwa na matatizo na Wajerumani wamekandikwa mabao tisa katika mechi nne pekee za kimataifa zilizopita, ambapo tatu kati ya hizo walishindwa na moja wakatoka sare.

"Tunatakiwa tujenge hisia miongoni mwa wapinzani wetu kwamba ukicheza dhidi ya Ujerumani basi hauko salama, hata katika dakika ya 93," Watzke alisema.

(rtre)