1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujenzi wa Ujerumani Mashariki: Fedha na maneno mazuri

3 Oktoba 2010

Wakati Ujerumani Mashariki inaungana tena na Ujerumani Magharibi miaka 20 iliyopita, palikuwa na matumaini makubwa kwamba kwa kipindi kifupi uchumi wa pande hizi mbili ungelitangamaa na nchi nzima kuwa na viwango sawa.

https://p.dw.com/p/PLbJ
Magdeburg (Sachsen-Anhalt): Den Schriftzug: "Gemeinschaftswerk Aufschwung Ost" an einer verwitterten Schallschutzwand in Magdeburg passieren am 07.04.2004 zwei Menschen (Illustration zum Thema Aufbau Ostdeutschland, strukturschwache Ost-Gebiete)
Shughuli za ujenzi mpya sehemu ya maendeleo ya kiuchumi ya upande wa mashariki katika mji wa MagdeburgPicha: dpa ZB-Fotoreport

 Hadi sasa zimeshatumika Euro bilioni 1.3 kuijenga upya Ujerumani Mashariki, lakini kama anavyosema mwandishi wetu, Sabine Kinkartz, kuigeuza Mashariki kuwa kama Magharibi bado kutachukuwa muda mrefu.

Sura ya Sasa ya Mashariki

Ikiwa mtalii wa Ujerumani Magharibi Magharibi atatembelea miji ya Ujerumani Mashariki hivi sasa, bila ya shaka atavutiwa na hali ya usafi wa nyumba zake, unyororo wa barabara zake, na usasa wa miundombinu yake. Si ajabu akijiuliza, hivi kwani kilichobakia kujengwa hapa ni kipi tena? Baada ya miaka 20 ya kuifufua sehemu hii ya Ujerumani, bila ya shaka mtu ana mengi mapya ya kujionea. Japokuwa kuna wanaoona kuwa ufufuaji huu umechukuwa muda  mrefu zaidi kuliko ilivyotegemewa, aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Ujerumani Mashariki wakati nchi hii inaungana, Lothar de Maizière, anaamini kuwa mafanikio ni makubwa sana.  

"Mwanzoni hatukudhani kabisa kama mambo yangekwenda haraka hivi. Lakini leo mtu asiyeona namna nchi inavyostawi, basi ama ni kipofu au ni mpumbavu", anasema de Maizière. "Leo hii ninapopita maeneo ya Görlitz, kupitia Quedlinburg na maeneo mengine tele, najiuliza kimoyomoyo, miji hii imekuwaje." 

Görlitz Stadtsanierung
Eneo la mjini GörlitzPicha: AP

Gharama Kubwa?

Gharama halisi ya Muungano wa Ujerumani hadi sasa inaweza kutajwa kwa hesabu tu. Kiasi ya Euro bilioni 1.3 zimeshatolewa katika kipindi cha baina ya mwaka 1991 na 2009, ambapo sehemu kubwa ya fedha hizi zimekwenda kwenye miradi ya ujenzi wa miundombinu ya nyumba, barabara na maji.


Lakini, juu ya yote, kilichokuwa kinahitajika Ujerumani Mashariki si ujenzi wa miundombinu tu, bali kwa hakika hasa uchumi wote wa sehemu hii ya Ujerumani ulikuwa umeshavurugika kufikia wakati Muungano unatokea. Tatizo la ukosefu wa ajira lilikuwa kubwa mno kupindukia ukilinganisha na Magharibi, thamani ya fedha yake ilikuwa imeporomoka chini kabisa na uzalishaji wa viwandani ulikuwa ni kama vile umesita. Kwa hivyo robo moja ya zile Euro bilioni 1.3 zilipaswa kutumika katika mambo mengine ya uimarishaji wa uchumi, mbali na ujenzi na uimarishaji wa miundombinu

Kuunganisha Sarafu Lilikuwa Jambo la Lazima

Wiedervereinigung: West-Auto frisst Ost-Trabant. D-Mark
Muungano na Deutsch Mark:Gari la Magharibi likachukua nafasi ya lile la Mashariki-TrabantPicha: AP

Katika kunusuru hali isizidi kuwa mbaya, ikawa ni lazima sasa sarafu iunganishwe na sasa iwe moja baina ya Mashariki na Magharibi. Wataalamu wa masuala ya fedha wakapigania hilo na hatimaye likafanikiwa ingawa kwa upinzani mkali. Anakumbuka waziri wa fedha ya Shirikisho la Ujerumani wa wakati huo, Theo Waigel, kwamba palikuwa na msemo kwenye wizara yake: "Deutsch Mark haiji kwetu, tunakwenda kwake." Ndani ya wizara yake kulikuwa na kila mawazo na maoni ya namna gani ya kuliendea suala hili la thamani ya sarafu wakati wa Muungano, lakini baadaye wote walifahamu kwamba hapakuwa na njia nyengine mbadala isipokuwa kuunganisha thamani ya fedha.


Biashara Mbovu?

Helmut Kohl (M) winkt bei einer Wahlkampfveranstaltung der konservativen "Allianz für Deutschland" auf dem Erfurter Domplatz der Menschenmenge zu, die unzählige Deutschlandfahnen schwenkt (Archivfoto vom 20.02.1990). Bei seinem ersten Wahlkampfauftritt in der DDR jubelten Kohl rund 130.000 DDR-Bürger zu. Kohl unterstützte das aus der DDR-CDU, der neu gegründeten Gruppierung Demokratischer Aufbruch (DA) und Deutsche Soziale Union (DSU) bestehende Bündnis für die DDR-Volkskammerwahlen am 18. März 1990. Foto: Heinz Wieseler dpa/lbn (zu Serie Deutsche Einheit - dpa 4013 vom17.03.2010 ) +++(c) dpa - Bildfunk+++
Kansela wa Shirikisho Helmut Kohl akiwapungia wapiga kura wakati wa kampeni ya uchaguzi mjini ErfurtPicha: picture alliance/dpa

Theo Waigel,Waziri wa zamani wa Fedha, katika serikali ya Helmut Kohl lazima alikumbana na suali gumu lilitokana na wasiwasi wa Mmarekani mmoja ikiwa "ununuzi" wa Ujerumani Mashariki haukuwa biashara mbaya. "Hili nilikuwa nikilisema mara kwa mara kwamba, ndiyo jambo hili linachukuwa muda mrefu na gharama kubwa zaidi kuliko tulivyolitegemea, lakini leo hii watu milioni 18 wanaishi kwa uhuru na kidemokrasia. Na ikiwa nanyi (Wamarekani) mutaweza kuleta faida kama hiyo kwa Irak baada ya miaka kumi, mutaweza kujiuliza vyema zaidi swali hili."

Leo hii, mfanyabiashara huyo anasema kwa sauti ya chini: "Theo, sitalirudia tena suali lile kamwe." Hii ni kwa kuwa ujenzi wa Ujerumani Mashariki ni hatua kubwa ya kuonesha mshikamano, ambao ni shida kuupata nje ya mipaka ya Ujerumani. Mshikamano ambao umezifanya raha na shida za Wajerumani ziwe moja, ama wawe wanatoka Mashariki au Magharibi.

Na mkakati huu wa ujenzi wa Ujerumani Mashariki unatarajiwa kuendelea hadi mwaka 2019. Hii maana yake ni kusema kwamba, katika miaka ijayo bado fedha zitaendelea kutoka Magharibi kuelekea Mashariki. Ama kitakachotokea baada ya hapo, ni suala la kusubiri na kuona, lakini kwa ujumla tangu Ujerumani ilipoungana tena umekuwa ni wito wa taifa moja kupambana na umasikini popote pale ulipo. 

Mwandishi: Kinkartz,Sabine/Khelef,Mohammed

Mhariri: Abdulrahman,Mohamed