1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza: Maji yaufika shingoni uongozi wa Liz Truss

Daniel Gakuba
20 Oktoba 2022

Mambo yanazidi kuwa mabaya kwa waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss, baada ya waziri wa mambo ya ndani kujiuzulu na wabunge wa chama chake kuishutumu serikali yake kukiaibisha chama na kukielekeza katika mgogoro.

https://p.dw.com/p/4ISNQ
Großbritannien | Liz Truss
Waziri Mkuu Liz Truss wa Uingereza anayekabiliwa na shinikizo kubwaPicha: Leon Neal/Getty Images

Waziri wa mambo ya ndani aliyejiuzulu jana jioni, Suella Braverman alikuwa wa pili muhimu kuondoka katika baraza la mawaziri la Waziri Mkuu Liz Truss, baada ya waziri wa fedha Kwasi Kwarteng kufungishwa virago siku tano zilizopita.

Soma zaidi: Truss aomba radhi kwa makosa lakini hatazamii kujiuzulu 

Kwarteng, mshirika wa karibu kisiasa wa Bi Truss aliponzwa na bajeti ndogo aliyoitangaza, ambayo iliitumbukiza Uingereza katika mgogoro mkubwa wa kifedha na kukosolewa vikali kutoka ndani na nje ya Uingereza.

Kikao cha jana cha bunge cha maswali na majibu kwa waziri mkuu Liz Truss kilizidisha masaibu ya waziri mkuu huyo ambaye hajadumu madarakani hata kwa miezi miwili.

Kura juu ya kurejeshwa kwa utaratibu wenye utata wa kuchimbwa gesi chini ya miamba, inayoungwa mkono na waziri mkuu lakini ikipingwa vikali na chama cha upinzani cha Labour na wabunge wengi wa chama tawala cha Conservative ndio ilikuwa kiini cha mzozo.

England | Parteitag der Konservativen in Birmingham | Kwasi Kwarteng
Masaibu ya lianza na bajeti ndogo iliyotangazwa na aliyekuwa waziri wa fedha, Kwasi Kwarteng (pichani) ambaye alitimuliwaPicha: Kirsty Wigglesworth/AP Photo/picture alliance

Liz Truss ajitutumua, asema hang'oki mtu

Bi Truss aliyekuwa ametetereshwa na hatua ya waziri wake mpya wa fedha kufutilia mbali mipango yote ya uchumi iliyokuwa ahadi za kampeni ya serikali yake, alijitutumuwa bungeni pale upinzani uliposema ikiwa sera zake zimeshindwa, yeye pia anapaswa kufungasha virago. Truss alisema hang'oki.

Alisema, ''Bwana Spika, mimi ni mpambanaji, siendi kokote. Maamuzi yangu ni kwa maslahi ya taifa, kuhakikisha tunao utengamano kiuchumi.''

Soma zaidi: Jeremy Hunt afuta mipango ya kupunguzwa kodi 

Wabunge wa Conservative walitishiwa kufukuzwa chamani iwapo wangeungana na upinzani kuipitisha kura, huku mnadhimu mkuu wa chama hicho tawala akisema kura hiyo ingechukuliwa kama ya imani kwa serikali, kwa maana kwamba kama kura hiyo ingepita, waziri mkuu Liz Truss angeondoka.

Mwishowe chama cha Conservative chenye wingi wa viti bungeni kilishinda, lakini namna wabunge wa walivyoshinikizwa iliacha mgawanyiko mkubwa.

Jahreskonferenz der britischen Konservativen Tory Partei in Birmingham
Mtafaruku katika uongozi wa chama cha Conservative umekipokonya umaarufu miongoni mwa wapiga kuraPicha: Jacob King/AP/picture alliance

Mparaganyiko miongoni mwa wabunge wa chama cha Conservative

Yalikuwapo madai ya baadhi ya wabunge, kuwa mabavu yalitumika kuwashinikiza wahafidhina kumuunga mkono waziri mkuu. Hali hiyo iliwafanya baadhi ya wabunge wa muda mrefu wa chama hicho kusema wamepoteza imani na mwelekeo wa chama chao, na kutaka wazi wazi waziri mkuu atimuliwe.

Mmoja wa wabunge hao ni Gary Streeter, ambaye kupitia mtandao wa twitter alisema kuwa hata ikiwa wataweza kumbandua Liz Truss, chama cha Conservative kitahitaji muujiza kuweza kurejesha nidhamu na kuiongoza ipasavyo Uingereza.

Soma zaidi: Waziri Mkuu Uingereza ahaha kurejesha imani baada ya kuvurunda

Shinikizo dhidi ya waziri mkuu huyo limeendelea leo baada ya mbunge mwingine wa chama chake, Sheryll Murray kuarifu kuwa amewasilisha kwenye kile kiitwacho kamati ya 1922, barua yake ya kutokuwa na imani na uongozi wa Liz Truss.

Kamati hiyo ndio yenye dhamana ya kuweka utaratibu wa kuwabadilisha viongozi wa chama cha Conservative.

Vyanzo: rtre, ape