1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNigeria

Uhaba wa mafuta,pesa vyatia doa kampeni ya uchaguzi, Nigeria

15 Februari 2023

Uhaba wa mafuta na matatizo ya upatikanaji wa pesa taslimu vinavyoshuhudiwa Kaskazini mwa Nigeria, vimeitia dosari kampeni ya uchaguzi inayoendelea maeneo hayo.

https://p.dw.com/p/4NUmt
Nigeria Wahlen 2023
Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP

Mapema asubuhi, raia katika mji wa Kano, Kaskazini mwa Nigeria walijawa na hasira wakati wakigombea nafasi ya kujiorodhesha kuwa miongoni mwa wateja watakaoruhusiwa kwa siku hiyo kutoa pesa. Muda mrefu hata kabla ya Benki hiyo kufungua milango yake, umati wa watu ulikuwa umekusanyika wakiwa na shauku ya kutoa pesa taslimu, ambapo serikali iliweka kikomo kwa kila raia kutoa naira 10,000 ambayo ni sawa na dola 20 pekee kwa siku.

Kilichosababisha hali hiyo, ni mpango wa serikali wa kubadilisha noti za zamani kwa muundo mpya, jambo lililopelekea sintofahamu na kupunguza mzunguuko wa pesa na hivyo kusababisha uhaba wa pesa. Karibu na benki hiyo, mamia ya magari na pikipiki yalikuwa yameegesha tangu asubuhi na mapema nje ya vituo vya mafuta yakisubiri kupatiwa huduma kufuatia uhaba mwingine unaoshuhudiwa ambao ni wa mafuta.

Taharuki miongoni mwa raia wa Nigeria

Nigeria Wahlen 2023
Wafuasi wa Mgombea wa Chama cha Upinzani PDP, Atiku Abubakar wakiwa katika kampeni huko Kano, NigeriaPicha: Pius Utomi Ekpei/AFP

Takriban wiki mbili kabla ya uchaguzi wa kumsaka mrithi wa Rais Muhammadu Buhari, uhaba huo katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, umeififiza kampeni, kuwakera wapiga kura na kusababisha taharuki katika maandalizi ya uchaguzi.

Wiki iliyopita, ghasia zilizuka kutokana na uhaba wa fedha wakati Buhari alipotembelea jimbo la Kano, mojawapo ya ngome zake na uwanja muhimu wa mchuano katika chaguzi hizi ikiwa pia na idadi kubwa ya pili ya wapiga kura waliojiorodhesha.

Soma zaidi: Nigeria yasema uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa

Nigeria Wahlen 2023/Präsidentschaftskandidat Atiku Abubakar
Mgombea Urais wa Chama cha Upinzani PDP, Atiku AbubakarPicha: Pius Utomi Ekpei/AFP

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) Mahmood Yakubu aliwahakikishia Wanigeria siku ya Jumatano kwamba uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa Februari 25, huku kukiwa na wagombea watatu wakuu wa nafasi ya urais wakiwa katika kinyang'anyiro kikali.

Lakini akitazama msururu wa watu nje ya benki za Kano, mfanyabiashara wa masoko Mohammed Ali Danazumi amesema uchaguzi haupo katika mawazo yake. Alikuwa akisubiri kwa muda wa masaa mawili ili kuweza kutoa pesa taslim baada ya kushindwa kufaanikisha azma yake hiyo siku iliyotangulia. Danazumi amesema uhaba wa mafuta na pesa taslim tayari vimesababisha hali mbaya kabla ya uchaguzi wa rais wa Februari 25, 2023.

Vyama vya siasa vyatupiana lawama

Nigeria | Verleihung der Nationalen Ehrenauszeichnung
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: Ubale Musa/DW

Chama tawala cha Buhari cha All Progressives Congress (APC) na chama kikuu cha upinzani cha Peoples Democratic Party (PDP) wanatupiana shutuma za njama na hujuma kwa lengo la kujipatia kura. Baadhi ya vigogo wa APC wamemtuhumu mpinzani wao Bola Tinubu ambaye ni gavana wa zamani wa jiji la Lagos na anayewania pia kiti cha Urais kwa kusababisha uhaba huo wa fedha.

Soma zaidi: Nigeria yaweka kikomo cha utoaji pesa zilizopo benki 

Wiki iliyopita, Buhari ambaye anaondoka madarakani baada ya mihula miwili, aliwataka Wanigeria kumpa siku saba kupatia ufumbuzi uhaba huo wa pesa, ambao amelaumu kuwa unatokana na uzembe na vitendo vya baadhi ya watu kujilimbikizia pesa katika zoezi hili la usambazaji wa noti mpya. Siku ya Ijumaa, Buhari amefanya mkutano wa dharura kuhusu uhaba wa fedha na maafisa wakuu, lakini magavana wa APC tayari walimuonya kuwa wana wasiwasi kuhusu athari kwenye uchaguzi huo.

Nigeria na historia mbaya ya uchaguzi

Nigeria | LNG Anlage
Kiwanda cha mafuta yaliyosindikwa katika kisiwa cha Bonny, NigeriaPicha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Nigeria ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta ghafi barani Afrika, lakini haina uwezo wa kuyasafisha na hivyo hulazimika kuagiza mafuta inayotumia kutoka barani Ulaya na kwengineko. Tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999, chaguzi za Nigeria mara nyingi zimekuwa zikikumbwa na ghasia, ununuzi wa kura au matatizo ya vifaa.

Uchaguzi wa mwaka 2019 ulicheleweshwa kwa wiki moja. Jimbo la Kano kwa muda mrefu limekuwa na jukumu muhimu katika uchaguzi wa Nigeria. Buhari alichaguliwa mwaka 2015 na kuchaguliwa tena mwaka wa 2019 kutokana na wingi wa kura kutoka jimbo hilo la kaskazini magharibi.