Uganda yatangaza kusambaa homa ya nyani
2 Septemba 2024Mamlaka za afya sasa zimo mbioni kudhibiti kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo ambapo hofu ni mashaka ni kwamba ni kipindi cha likizo ya shule na watoto wamerudi makwao wakisafiri kutoka sehemu moja ya nchi hadi nyingine.
Tarehe 24 mwezi Julai mwaka huu, kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Homa ya Nyani kiliripotiwa kwenye mji wa Bwera wilaya ya Kasese mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ijapokuwa wizara ya afya ilihakikisha kuwa ilikuwa imeweka mikakati ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, sasa imetangaza kwamba ugonjwa huo umesambaa sehemu mbalimali za nchi a huenda idadi ya waathirika ikawa kubwa.
Luteni Kanali Henry Kyobe ambaye ndiye husimamia masuala ya miripuko katika wizara hiyo amethibitisha visa hivyo na kuhimiza umma kuwafichua mapema wale walio na ishara za ugonjwa huo.
Soma pia: Kenya yarekodi kisa cha kwanza cha maradhi ya mpox
Pia ametoa mwito kutowanyanyapaa waathirika kwani hii itawapelekea kujificha wasipate matibabu na kuendelea kusambaza ugonjwa huo.
"Tunafanya kila juhudi kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo lakini tunahimiza dhidi ya uyanyapaa kwa wagonjwa hao"
Kwa mujibu wa wizara hiyo kuna angalau mwaathrika mmoja katika kila kanda ya nchi Kaskazini, Magharibi, Mashariki na Kati mwa nchi.
Miongoni mwa kile kinachoelezewa kuchangia maambukizi ni mienendo ya ngono ya waendeshaji wa magari ya mizigo. Dereva mmoja wa Kenya aliyegunduliwa kuwa na ugonjwa huo nchini kwao alikuwa ametokea Uganda akielekea Rwanda kuoitia nchi hiyo.
WHO Uganda: Toeni taarifa za wagonjwa
Kulingana na afisa mkuu wa Shirika la Afya Duniani mjini Kampala, Dkt Annet Alenyo, ishara za ugunjwa huo hudhihirika kwa awamu tatu.
Ya kwanza ni kuumwa na kichwa, udhaifu na homa mwilini, kutetemeka na kuwa na koo inayowasha. Wiki iliyopita wanakijiji huko Busia walikumbana na ishara hizo baada ya mtu mmoja kufariki na hadi sasa wanahofia kuwa ni Homa ya Nyani.
Awamu ya pili ni pale vipele vinapojitokeza na kusambaa kwa mwili wote.
"Awamu ya pili ya ugonjwa huo ni kuonekana kwa vipelepele vyenye maji maji kama ya aliyechomwa maji ya moto." Alisema Dkt Kyobe
Ili kuepusha kusambaa kwa ugonjwa huo, watu wanahimizwa kunawa mikono kila wakati na pia kutoshiriki ngono na watu waliofahamikiana nao vyema.
Soma pia: WHO: Chanjo za mpox kuwasili hivi karibuni nchini DRC
Kile ambacho bado kinashagaza ni kwa nini chanjo dhidi ya ugonjwa huo zimechelewa kufikishwa katika maeneo hatari kama vile kwenye mpaka wa Uganda na Kongo ambayo imeripoti vifo vya watu 35.