Uganda yapinga kuondolewa AGOA
8 Januari 2024Hatua ya Marekani ambayo imeanza kutekelezwa mwezi huu wa Januari inaikosesha Uganda kiasi cha dola milioni 200 kama mapato kutokana na bidhaa ambazo zimekuwa zikiuzwa nchini Marekani.
Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, Marekani ilitisha kuiondoa Uganda kwenye mkataba wa AGOA ambao unatoa fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kisiasa kati ya Marekani na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, na kutoa ushauri kuwa ingebadili msimamo wake kama Uganda ingetoa ufafanuzi kuhusu jinsi inavyopanga kuboresha haki za binadamu pamoja na kufutilia mbali sheria yenye utata dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja kufikia mwezi Januari.
Uganda imeshikilia kuwa haitashurutishwa kubadili msimamo wake wa kulinda hadhi na utamaduni wa Kiafrika na kwa mujibu wa maumbile.
Soma pia: Kundi la wanamgambo la ADF lawauwa watu watatu Uganda
Wiki iliyopita Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza kwamba Uganda itakuwa miongoni mwa mataifa ambayo yameondolewa kwenye mkataba huo wa kibiashara wa masharti nafuu. Hii ina maana kuwa Uganda imepoteza soko la bidhaa zake mbalimbali ikiwemo zile za vitu vya sanaa, viungo, ngozi na kadhalika.
Msimamizi wa mkataba huo nchini Uganda Susan Muhwezi ametoa ufafanuzi zaidi, ''AGOA ni muhimu sana kwa Uganda, kwani wakituondoa itaamaanisha watu watapoteza ajira na mapato katika sekta hasa za nguo na kahawa. Naisihi serikali ya Marekani inayoongozwa na Rais Joe Biden ilizingatie hilo.''
Marekani ilitia saini mkataba wa kibiashara kati yake na Afrika mwaka 2004
Mataifa mengine ambayo yameondolewa kwenye mkataba wa AGOA kuanzia Januari mosi ni Gabon, Niger na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Bidhaa zinazohusishwa ni zile ambazo zimetengenezwa ndani ya nchi hiyo na zenye manufaa ya moja kwa moja kwa raia wa nchi hiyo. Chini ya mpango huo, Uganda ilikuwa ikishiriki biashara ya dola milioni 200 za Kimarekani kila mwaka.
Lakini kwa mtazamo wake, mbunge wa upinzani Asuman Basalirwa, amesema Uganda inaweza kupata masoko mengine kuziba pengo hilo, ''Badala ya Marekani tunaweza kupata masoko mengine kwa bidhaa zetu, tuache kudhani kwa Marekani ndiyo soko tu kwani kuna masoko Mashariki ya Kati na bara la Asia na hata Urusi.''
Susan Muhwezi kwa upande wake amesisitiza kuwa haifai kwa Marekani kuzihusisha haki za binadamu pamoja na suala la watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na biashara ambazo husaidia raia wa kawaida. ''Eti ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Sina habari kwamba Uganda inakiuka haki za binadamu.''
Soma pia: Jeshi la Uganda latangaza donge nono kuwanasa ADF
Mbunge Asuman Basalirwa naye anatoa mtazamo wake. ''Wasitulazimishe kufanya mambo kinyume na hadhi yetu, kwa sababu ya kutupa nafasi ya kuuza bidhaa zetu.''
Mkataba wa AGOA umekuwepo tangu mwaka 2000 na unayahusisha mataifa 36 yaliyosaini mkataba wake ambao utamalizika mwaka 2025. Zaidi ya bidhaa 1,800 zilisajiliwa kuhusishwa katika bishara hiyo yenye masharti nafuu na Marekani.
Mataifa mengine ya Afrika Mashariki ambayo yamo kwenye orodha hiyo ni Kenya, Tanzania na Rwanda ila Rwanda iliondolewa kwenye orodha ya kuuza nguo katika soko la AGOA mwaka 2018, wakati ilipopiga marufuku biashara ya nguo za mitumba ambazo kwa kiasi kikubwa hutokea Marekani.