Uganda yakabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi wa Congo
15 Novemba 2023Kundi hilo la wakimbizi zaidi ya elfu moja, wengi wao wakiwa wanawake na watoto waliingia Uganda Jumanne wiki hii wakielezea kuyakimbia mashambulizi ya kundi la waasi wa ADF.
Baadhi ya wakimbizi wamesimulia kuhusu mauaji ya raia yaliyofanyika katika mashambulizi hayo katika kijiji cha Kikyanga eneo la Beni wakisema kuwa watu wapatao 16 waliuawa.
Wakimbizi hao wametembea kwa miguu na kukabiliana na hali ngumu ya mvua na mafuriko ambayo yanalikumba eneo hilo.
Uganda kuwasamehe waasi wa ADF wanaojisalimisha
Kwa sasa shirika la msalaba mwekundu na viongozi wa wilaya ya Bundibugyo wanafanya kila juhudi kuwapa wakimbizi hao misaada ya kiutu ikiwemo chakula, maji na dawa.
Misaada hiyo ni haba kwa sasa kutokana na kupungua kwa ruzuku inayotolewa na mataifa wafadhili ambayo yanazingatia zaidi wahanga wa vita wa Ukraine na Urusi.
Baadhi ya wakimbizi wanahifadhiwa na jamaa na marafiki zao upande wa Uganda kwa hiyo idadi kamili ya walioingia Uganda bado haijathibitishwa.