Ufaransa mwenyeji wa mkutano wa mataifa ya Mediterania
10 Septemba 2020Kundi la EuroMed7 ni kundi ambalo si rasmi la mataifa saba ya Umoja wa Ulaya yanayopakana na bahari ya Mediterania, baadhi ya nyakati yakijulikana kama " klabu ya Med", ambayo yalifanya mara ya kwanza mkutano wao mwaka 2016 na ambayo hayaijumishi Uturuki.
Lakini mkutano huo katika kisiwa cha Ufaransa cha Corsica kitawaleta pamoja viongozi wa Ufaransa, Italia, malta, Ureno na Uhispania pamoja na wanachama wa Umoja wa Ulaya wa mataifa ya mashariki mwa bahari ya Mediterania Ugiriki na Cyprus.
Ufaransa imeiunga mkono kwa nguvu Ugiriki na Cyprus katika mkwamo unaoongezeka pamoja na Uturuki kuhusiana na maliasili ya gesi na mafuta pamoja na ushawishi wa jeshi la majini katika eneo la mashariki mwa Mediterania ambao umezusha hofu za mzozo.
Mkutano huo utafanyika leo mchana katika mji wa pwani wa kitalii nje kidogo ya mji mkuu wa jimbo la Corsica, Ajaccio.
Lengo la mazungumzo hayo ni "kupiga hatua katika kupata muafaka juu ya uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Uturuki ikiwa pamoja na yote kabla ya mkutano wa Septemba 24-25 wa Umoja wa Ulaya," afisa wa ofisi ya rais wa Ufaransa amesema.
Mshirika muhimu
Akisisitiza sera ya Macron kuelekea Uturuki, afisa huyo alisema kuwa Ufaransa inataka "ufafanuzi " katika uhusiano na Ankara ambayo inapaswa kuwa "mshirika muhimu."
Uturuki imetaka kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa zaidi ya nusu karne sasa na wakati juhudi zake za kuwa mwanachama zimekwama vibaya katika miaka michache iliyopita, na haionekani tena kuwezekana katika baadhi ya sehemu, inabaki kuwa mgombea wa kujiunga na kundi hilo la mataifa.
Utafutaji wa Uturuki wa gesi na mafuta katika eneo la maji linalodaiwa na Ugiriki kuwa ni lake umeathiri pa kubwa uhusiano kati ya mataifga hayo mawili wanachama wa NATO.
Uturuki mwezi uliopita iliweka vyombo vya utafutaji wa mafuta na gesi , meli ya Oruc Reis katika eneo la maji kati ya Ugiriki na Cyprus, hali iliyosababisha Ugiriki kufanya mazowezi ya kijeshi baharini.
Baadhi ya mataifa wanachama yatataka kuiwekea vikwazo Uturuki katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, ambapo waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisema mwishoni mwa juma hatua kama hizo ziko mezani.