Twitter kuanza kuwafuta kazi wafanyakazi wengi Ijumaa
4 Novemba 2022Hayo ni kulingana na taarifa ya ndani kwa wafanyakazi. Wafanyakazi wengi wa kampuni hiyo wamewasilisha mashtaka dhidi ya hatua hiyo wakidai mmiliki mpya bilionea Elon Musk anakiuka sheria ya kazi.
Barua pepe ya kampuni hiyo iliyotumwa kwa wafanyakazi wake na ambayo shirika la habari la AFP limepata nakala yake, ilieleza kwamba wafanyakazi watapokea barua pepe binafsi kuanzia Ijumaa kuhusu hatima yao katika kampuni hiyo. Iliwataka wafanyakazi wote waende nyumbani na wasiripoti kazini Ijumaa asubuhi. Kwamba afisi zao zitafungwa na baji za kielektroniki za kuingia hazitaweza kufanya kazi.
Barua pepe hiyo ilisema katika juhudi za kuiweka Twitter katika njia nzuri, tutapitia mchakato mgumu wa kupunguza idadi ya wafanyakazi wetu.
Haikutoa idadi kamili ya wafanyakazi watakaopigwa kalamu lakini magazeti ya Marekani ya Washington Post na New York Times yameripoti kwamba takriban nusu ya idadi jumla ya wafanyakazi 7,500 wa kampuni hiyo watafutwa kazi.
Wafanyakazi wa Twitter wamekuwa wakitarajia hali kama hii tangu bilionea Elon Musk alipoinunua kampuni hiyo kwa dola bilioni 44 wiki iliyopita na kwa haraka akaivunja bodi yake ya usimamizi kando na kumfuta kazi mkurugenzi mkuu na wengine waliokuwa mameneja watendaji.
Twitter yashtakiwa kwa kuwafuta kazi wafanyakazi kinyume cha sheria
Jana Alhamisi wafanyakazi watano wa Twitter ambao walishafutwa kazi waliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya kampuni hiyo kwa misingi ya walivyotimuliwa.
Kwenye malalamishi yao walidai hawakupewa ilani ya muda wa siku 60 inayohitajikwa chini ya sheria ya kazi nchini humo na Marekani na katika jimbo la Carlifornia.
Kulingana na hati ya mashtaka, wafanyakazi hao wameitaka kampuni ya Twitter kuzuiwa kuwataka wafanyakazi wake kusaini hati zitakazoondoa haki zao.
Baadhi ya wafanyakazi walikosoa pakubwa mchakato wa kampuni hiyo kuwatimua. Taylor Leese, meneja wa timu ya uhandisi aliyedai alifutwa kazi amesema, "hatua hii ya kuwafuta watu kazi katika Twitter ni kichekesho na inaaibisha. Washirika wa Musk ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Tesla wanafanya maamuzi juu ya wafanyakazi ambao hawajui chochote kuwahusu." Leese ameongeza kuwa ni hali ya kusikitisha sana.
Musk alighadhabishwa na ununuzi wa Twitter kwa fedha za kupindukia
Akionekana kuhuzunishwa na ununuzi wake wa Twitter, ambayo Musk alisema alilipa kupindukia, bwenyenye huyo anatafuta njia za kurejesha fedha zake tena kwa haraka.
Wazo lake la hivi karibuni la kupata fedha kupitia Twitter lilikuwa watumiaji wa Twitter waliopewa baji blue ya watozwe dola nane kila mwezi.
Mpango wa Musk na Twitter wazusha hofu ya ukiukaji Asia, Mashariki ya Kati
Baadhi ya kampuni kubwakubwa ulimwenguni ikiwemo ya magari Volkswagen, General Motors na General Mills zilisitisha matangazo yao ya kibiashara kwenye Twitter mnamo wakati shinikizo linaongezeka kwa Musk anapojaribu kuubadilisha mtandao huo kuwa wa kibiashara zaidi.
Maafisa na wanaharakati wameelezea wasiwasi wao kwamba Musk ataruhusu matamshi ya chuki na upotoshaji kuendelezwa bila kudhibitiwa kwenye mtandao huo na pia kurejesha kurasa ambazo zilishapigwa marufuku ikiwemo yake rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
( AFP)