1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Musk na Twitter wazusha hofu ya ukiukaji

29 Aprili 2022

Bilionea wa Kimarekani Elon Musk ahahidi kulegeza masharti ya maudhui, licha ya Twitter kuwa kikwazo kwa viongozi wa serikali kwenye nchi ya Mashariki ya kati. Wakosoaji mitandaoni wana mashaka na ahadi ya Musk.

https://p.dw.com/p/4AcmJ
Karikatur | Twitter-Symbol mit dem Kopf von Elon Musk mit Sprechblasen "Twi, twi".
Picha: Sergey Elkin

Bilionea Elon Musk amenunua mtandao wa kijamii wa Twitter kwa pesa taslimu dola bilioni 44, na kuahidi kulegeza masharti ya maudhui yanayotumwa kwenye mtandao huo, lakini wakosoaji wanasema hii inaweza kuwa changamoto katika nchi za Mashariki ya Kati ambako viongozi wa serikali hutumia mitandao ya kijamii kufuatilia wapinzani na kueneza taarifa za uongo. 

Twitter na Facebook ni mitandao ya kijamii iliyotuhumiwa kwa uchochezi na kuathiri maisha ya watu  wakati wa machafuko kwenye nchi za Kiarabu mwaka 2011.

Serikali zilichukuwa hatua za kuwafunga wapinzani endapo zilikosolewa kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyopelekea ukandamizaji wa demokrasia.

Marc Owen Jones, mwandishi vitabu kuhusu nchi za  Mashariki ya Kati, na profesa msaidizi wa mafunzo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Hamad bin Khalifa nchini Qatar, anasema: "Twitter inatumika na  baadhi ya nchi kusambaza propaganda na kuwakandamiza wanaharakati, Umiliki wa Elon Musk kwa Twitter utazidisha matatizo kwenye eneo letu, na Twitter itatumika  kama chombo cha uchunguzi na ukandamizaji."

Elon Musk übernimmt Twitter
Musk ameahidi uhuru wa kujieleza kwenye TwitterPicha: Scott Olson/Getty Images

Twitter haikulijibu shirika la habari la Reuters ombi la kutoa maoni namna watakavyokabiliana na serikali za Mashariki ya Kati na kuwalinda wakosoaji wanaotoa maoni yao kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii.

Baadhi ya wanaharakati wa kisiasa wanatarajia uongozi wa Musk, kuwarejesha tena kwenye mtandao wa twitter watu waliopigwa marufuku, akiwemo rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump.

Mnamo 2020, maelfu ya watu kutoka Misri, Honduras, Indonesia, Saudi Arabia na Serbia, wanaoiunga mkono serikali, walifungiwa kutumia mtandao ya kijamii wa twitter.

Abdullah Alaoudh, mkurugenzi wa utafiti kuhusu demokrasia nchini Saudi Arabia, ni mmoja wa wanaharakati na wasomi waliokamatwa tangu Mwanamfalme Mohammed bin Salman kuanza mipango ya kurithi kiti cha ufalme cha baba yake mwaka 2017.

Alodah, ambaye ana wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, alikamatwa mnamo Septemba 2017 nyumbani kwake masaa machache baada ya kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter kuzitaka Qatar na Saudi Arabia kumaliza mzozo wa kidiplomasia. Hapo awali aliikosoa Riyadh kukandamiza  haki za binaadamu.

Mamlaka nchini  Misri zimewafungulia mashitaka wanaharakati kwenye mitandao, akiwemo mtetezi wa haki za binadamu, Hossam Bahgat, ambaye alitozwa faini ya paundi 10,000 za Misri baada ya kuituhumu tume ya uchaguzi kwa udanganyifu mnamo mwaka  2021.

Mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook imepigwa marufuku nchini Iran tangu 2009 kulipotokea maandamano ya kupinga serikali.

Viongozi wengi wa Iran wanatumia Twitter licha ya marufuku hiyo, huku wengi wakiwa na kurasa bandia nyingi zenye lugha mbalimbali kulingana na Kiongozi Mkuu Ayatollah Khamenei.

Meir Javedanfar, mhadhiri wa siasa za Iran katika chuo kikuu cha Reichman nchini Israel, anasema ." Twitter inapaswa kuanzisha teknolojia ambayo inawawezesha Wairani kufikia jukwaa hilo bila kukamatwa na mamlaka ya Iran.Vinginevyo, hakuna mtu nchini Iran anayejali ni nani anamiliki Twitter."

Mwandishi: Neema Misheki
Reuters