1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Uchaguzi Nigeria yakanusha kushawishiwa kisiasa

17 Februari 2019

Huku wagombea uchaguzi nchini Nigeria wakishutumiana kwa tangazo la ghafla la kuahirishwa uchaguzi, tume ya uchaguzi inasema kuwa tangazo hilo halikushinikizwa kisiasa wala kiusalama.

https://p.dw.com/p/3DWoo
Nigeria - Wahl verschoben
Picha: picture alliance/AP Photo/B. Curtis

Wagombea wakuu wa uchaguzi nchini Nigeria wanatupiana lawama kutokana na uamuzi wa ghafla uliochukuliwa na tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi wa rais kwa wiki moja hadi hapo tarehe 23 Februari, kila mmoja akimuotezea kidole cha lawama mwenzake, ingawa wote wakisisitiza haja ya utulivu.
 
Uamuzi huo uliotangazwa masaa matano tu kabla ya vituo vya kura kufunguliwa siku ya Jumamosi unatajwa kuigharimu nchi hiyo dola bilioni 2 za Kimarekani, sambamba na kuiathiri hadhi ya taifa hilo kubwa kabisa kufuata mfumo wa kidemokrasia barani Afrika.

Kwa sasa, mamlaka zinazohusika na uchaguzi zina kazi ya kuamua namna ya kuvifanya vifaa vya kupigia kura ambavyo tayari vilishawasilishwa kwenye vituo vya kupigia kura, huku hali ikiwa ya wasiwasi kutokana na matukio ya hivi karibuni ambapo majengo ya tume ya uchaguzi yalichomwa moto.

Tume ya Uchaguzi yakanusha kuingiliwa kisiasa

Nigeria Kano - Wahlplakate
Bango la uchaguzi kwa kampeni za Rais Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/dpa/AP/B. Curtis

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Mahmood Yakub, aliwaambia waangalizi, wanadiplomasia na waandishi wa habari kwamba kucheleweshwa huku kwa uchaguzi hakuhusiani na hali ya ukosefu wa usalama wala kuingiliwa kati kisiasa. Badala yake, mwenyekiti huyo alisema "mazingira mabara" ikiwemo hali mbaya ya hewa ndiyo iliyopekelea kuchelewa kwa ndege zilizobeba vifaa na pia moto kwenye ofisi tatu za tume yake.

Ikiwa uchaguzi ungelikwenda kama ulivyokuwa umepangwa, vituo vya kura visingeliweza kufunguliwa kwa wakati mmoja nchi nzima. "Ni muhimu sana kwa wananchi kuupokea uchaguzi ulio huru, wa haki na wenye kuaminika," alisema Yakub, akiongeza kwamba hadi saa nane usiku walikuwa na uhakika kwamba uchaguzi ungelifanyika, huku akihakikisha kuwa tarehe 23 Februari haina mjadala tena.

Wapigakura wenye hasira katika mji mkuu, Abuja, na kwengineko ambao walitoka majumbani kwao kwenda kupiga kura zao, wakiwemo raia wengi wa nchi hiyo wanaoishi mataifa ya nje, walisema wasingeliweza tena kubakia kwa siku saba nyengine na kuonya kwamba huenda watu wakagomea kupiga kura. Wengine walionesha hasira zao kutokana na kulazimika kupanga upya shughuli zao ikiwemo mitihani na harusi.

Wanasiasa washutumiana

Nigeria - Wahlkampf
Mabango ya kampeni kwenye mji wa Mubi.Picha: Getty Images/AFP/L. Tato

"Ikiwa tume ya uchaguzi ilijuwa kuhusu matatizo haya, kwa nini ilingojea hadi dakika za mwisho kutangaza kuahirisha uchaguzi?" Alihoji Godspower Egbenekama, msemaji wa chifu wa Gbaramatu kwenye jimbo la Delta. "Hii inaonesha kuna mtu analazimisha hili jambo mahala fulani."

Chama kinachomuunga mkono mgombea mkuu wa upinzani, Atiku Abubakar, kiliutuhumu utawala wa Rais Muhammadu Buhari kwa kuchochea tangazo la kuahirishwa kwa uchaguzi "kwa lengo la kuhakikisha kuna idadi ndogo ya wapiga kura." Hata hivyo, chama hicho kiliwatolea wito wapiga kura kujitokeza kwa wingi zaidi vituoni wakati uchaguzi utakapofanyika.

"Unaweza kuahirisha uchaguzi lakini huweza kuahirisha kudura," aliandika Abubakar kwenye mtandao wa Twitter.

Mwenyewe Buhari alisema amesikitishwa sana baada ya tume ya uchaguzi kuwa ilishatoa "hakikisho kila siku na takribani kila saa kwamba ilikuwa tayari kuandaa uchaguzi." Rais huyo alitoa wito wa utulivu huku akisisitiza kuwa utawala wake hauingilii kazi za tume hiyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP
Mhariri: Caro Robi