1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuhuma za upendeleo na ukabila katika serikali ya Kenya

Wakio Mbogho14 Aprili 2023

Baadhi ya maafisa wa serikali Kenya wanakabiliwa na madai ya kufanya uteuzi kwa upendeleo wa kikabila na mirengo ya kisiasa. Madai hayo yameibuka katika wakati joto la kisiasa linazidi kupanda nchini humo

https://p.dw.com/p/4Q4o8
Rais wa Kenya Ruto na naibu wake Gchagua
Serikali ya Kenya inakabiliwa na shinikizo kutoka upinzaniPicha: Simon Maina/AFP

Hivi karibuni Gavana wa kaunti ya Nakuru Susan Kihika alilazimika kuwapandisha jukwaani maafisa wake kwenye mkutano mmoja wa umma mjini Nakuru, baada ya kukosolewa na mbunge wa Rongai Paul Chebor kwamba uteuzi alioufanya kwenye serikali yake ya kaunti unaegemea jamii yake pekee. Gavana Kihika hakuficha ghadhabu yake kufuatia shutuma hizi.

Soma pia: Kenya yakabiliwa na upungufu wa sarafu ya dola

Tatizo la kucheleweshwa mishahara ya wafanyakazi wa umma nchini Kenya limepatiwa ufumbuzi?

Baadhi ya viongozi wameonekana kuunga mkono madai ya mbunge huyo wa Rongai. Akizungumza dhidi ya muingiliano wa kikazi, Alfred Mutai, mbunge wa Kuresoi Kaskazini, anasisitiza umuhimu wa kila kiongozi kupewa uhuru na nafasi ya kufanya kazi.

Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la magharibi wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kikabila katika uteuzi unaofanyika katika afisi za umma. Wakiongozwa na mbunge wa Saboti Caleb Amisi, wanataka mkurugenzi mkuu wa huduma ya vijana ya NYS, Matilda Sakwa kurejeshwa kazini.

"Wiki hii mkurugenzi mkuu wa NYS, Matilda Pamela Sakwa aliondolewa kwenye wadhifa wake kwa njia isiyofaa na Waziri Aisha Jumwa. Huu tunauona kama ubaguzi wa kijinsia na kisiasa. Tangu achukue hatamu hiyo, NYS imekuwa na mageuzi makubwa. Kumekuwa na mwenendo wa kuwafuta kazi maafisa kutoka makabila na vyama fulani vya kisiasa na nafasi zao kuchukuliwa au kupewa watu kutoka makabila na vyama fulani vya kisiasa.”

Mbunge huyo anasema mwenendo huu pia umebainika wazi katika teuzi za maafisa wa umma zinazowasilishwa bungeni.

"Orodha ya hivi maajuzi ya viongozi wa bunge iliyowasilishwa na serikali ya Kenya kwanza, na uteuzi wa makatibu wasimamizi wa wizara ni kutozingatia kwa ujasiri kanuni ya ujumuishi kama ilivyoratibiwa kwenye kifungu cha 10 cha katiba.”

Madai haya yanajiri licha ya Rais William Ruto kuelezea mara kwa mara kwamba amejitolea kuwahudumia Wakenya wote kwa usawa.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru