Tsunami yaipiga Japan
1 Januari 2024Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan lilisema tetemeko hilo la Jumatatu (Januari 1) lilikuwa na ukubwa wa 7.6 kwa kipimo cha Richter na miji iliyoathirika zaidi ni Toyama, Ishikawa na Niigata, yote kwenye kisiwa chake kikubwa cha Honshu katika mwambao wa magharibi wa Bahari ya Japan.
Shirika la habari la Urusi, TASS, limewanukuu mameya wa miji ya Vladivostok na Nakhodka wakitangaza tahadhari ya tsunami katika maeneo hayo yaliyo kwenye kisiwa cha Sakhalin.
Soma zaidi: Japan yasema vipimo vya maji kulikotiririshwa maji ya Fukushima havionyeshi madhara
Onyo la mawimbi yenye ukubwa wa mita tatu lilitolewa pia kwenye baadhi ya maeneo ya Korea Kaskazini na Korea Kusini.
Serikali mjini Seoul iliwataka wakaazi wa miji ya mwambao wa mashariki kuchukuwa hadhari ya kupanda kwa viwango vya bahari.
Watu watakiwa kuhama
Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan iliripoti matetemeko kwenye mwambao wa Ishikawa na maeneo yake ya karibu majira ya 10:00 jioni.
Mamlaka hiyo ilitowa onyo la kutokea tsunami kubwa katika mwambao wa Ishikawa na matetemeko ya kiwango cha chini kwenye maeneo mengine katika mwambao wa kisiwa kikubwa cha Japan, Honshu.
Soma zaidi: Japan kuanza kutiririsha baharini maji ya kinu cha Fukushima
Televisheni ya shirika la utangazaji la Japan, NHK TV, iliripoti mawimbi yaliyofika ukubwa wa mita tano na kuwataka watu wa maeneo hayo kukimbilia milimani au kwenye mapaa ya majengo yaliyo karibu nao haraka iwezekenavyo.
Televisheni hiyo ilisema mawimbi ya tsunami yanaweza kurudi tena huku matangazo ya tahadhari yakiendelea kutolewa hata baada ya saa nzima tangu tahadhari ya kwanza itolewe.
Matetemeko mengine kadhaa madogomadogo yalilipiga eneo hilo.
Vinu vya nyuklia viko salama
Msemaji wa serikali ya japan, Yoshimasa Hayashi, aliwaambia waandishi wa habari kwamba vinu vya nyuklia kwenye eneo hilo havijaripoti tukio lolote lisilo la kawaida, ingawa ni "muhimu kwa watu wa maeneo ya mwambao kuhama haraka iwezekenavyo."
Mawimbi ya tsunami ya ukubwa wa mita tatu yalipiga kwenye mwambao wa Nigita na maeneo mengine ya jirani na hapo.
Soma zaidi: Umoja wa Ulaya waondoa vikwazo vya vyakula vya Japan
Serikali ya Japan imeanzisha kituo maalum cha dharura kukusanya taarifa za matetemeko na tsunami na kuzisambaza haraka kwa raia, kwa mujibu wa Waziri Mkuu Fumio Kishida, aliyerejelea onyo la kuhamwa haraka kwa maeneo yaliyoathirika.
Japan ni taifa lililo kwenye eneo lenye uwezekano mkubwa wa kukumbwa na tsunami. Mwezi Machi 2011, tetemeko kubwa na tsunami yalisababisha madhara makubwa kwenye kinu kimoja cha nyuklia.
Vyanzo: AFP, AP, Reuters