Tshisekedi amtaja Kagame "adui" wa Kongo
5 Desemba 2022Huku mvutano huo ukiendelea kati ya marais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Kongo, waumini wa Kikatoliki waliandamana jana Jumapili (04.12.2022) kote nchini humo kupinga uchochezi wa Rwanda na unafiki wa jumuiya ya kimataifa.
Soma Zaidi:DRC na Rwanda zapata mwafaka kuhusu vita mashariki mwa DRC
Rais Félix Tshisekedi alitoa wito huo jana wakati akiwahutubia vijana wa Kongo kupitia ujumbe ulioundwa na mamia ya vijana kutoka mikoa 26 ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akiwaomba kutofautisha kati ya raia wa Rwanda na utawala wa Rais Paul Kagame.
Tshisekedi alisisitiza kwamba Wanyarwanda wanahitaji msaada wa Wakongo ili kujikomboa kutoka utawala huo kandamizi.
Alisema "Ni utawala wa Rwanda unaoongozwa na Paul Kagame ndio adui wa Kongo. Wanyarwanda ni ndugu zetu na wanahitaji msaada wetu kwani wamezibwa midomo. Wanahitaji msaada wetu ili kujikomboa, kutukomboa na kuiondoa Afrika mikononi mwa viongozi wa aina hii walio bado nyuma."
Kauli hizo kali za Rais Tshisekedi zimefuatia shutuma zilizotolewa na Rais Kagame wiki iliyopita ambapo alimshtumu Tshisekedi kwa kutaka kujinufaisha kisiasa kutokana na mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo kwa kuahirisha uchaguzi huku nchi yake ikilaumiwa kwa matatizo hayo.
Wakati huo huo, Wakristo wa Kikatoliki waliandamana mitaani jana Jumapili nchini kote, ili kulaani uvamizi dhidi ya nchi hii unaodaiwa kufanywa na Rwanda kupitia uasi wa M23. Kwa zaidi ya miezi mitano sasa, waasi hao ambao Kinshasa inawataja kama magaidi wanadhibiti mji wa Bunagana na maeneo mengine. Waandamanaji pia walishutumu unafiki wa jumuiya ya kimataifa kama alivyoeleza Padri Bruno Kabambu wa parokia ya Mtakatifu Gabriel.
"Pia tunakemea tabia za baadhi ya mashirika ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Afrika Mashariki na mengineo ambayo hayana haki. Maumivu ya vita dhidi ya ndugu zetu wa Mashariki yanatulazimu kuwatumia ujumbe wa huruma na mshikamano." Alisema Padri Kabambu.
Soma Zaidi: Waasi wa M23 wajitenga na mapatano ya kusitisha mapigano
Mvutano baina ya Kinshasa na Kigali bado ni wa hali ya juu licha ya juhudi za upatanishi kuongezeka ili kujaribu kuleta amani katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo Umoja wa Mataifa umeinyooshea kidole Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23.
Sikiliza Zaidi: