1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC na Rwanda zapata mwafaka kuhusu vita mashariki mwa DRC

24 Novemba 2022

Mazungumzo ya Angola kuhusu vita ya mashariki mwa Kongo yafanikiwa kupata makubaliano ya vita kusitishwa na waasi wa M23 kuondoka

https://p.dw.com/p/4JzV0
Angola Luanda | Treffen der Präsidenten Kagame (L)  Lourenco (C) und Tshisekedi
Picha: JORGE NSIMBA/AFP

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda zimefikia makubaliano ya kusitisha vita mashariki mwa Kongo.Makubaliano hayo yamefikiwa jana kwenye mkutano mdogo wa kilele uliofanyika mjini Luanda nchini Angola.

Makubaliano yaliyofikiwa maana yake ni kwamba huenda ni kufuatiwa na utekelezaji wa hatua ya kusitisha mapigano katika eneo la Mashariki mwa Kongo ambako kunashuhudiwa vita.Kama alivyoweka wazi waziri wa mambo ya nje wa Angola Tete Antonio.

Portugal | Tete Antonio | angolanischer Außenminister in Lissabon
Picha: João Carlos/DW

Kauli ya mkutano

''Mkutano mdogo wa kilele umefikia maamuzi yafuatayo-Kusitishwa vita kikamilifu na pande zote na hasa mashambulizi ya M23 dhidi ya jeshi la Kongo-FARDC na ujumbe wa Umoja wa mataifa Monusco kufikia Ijumaa tarehe 25 Novemba saa kumi na mbili kamili jioni.''

Kufikiwa kwa makubaliano haya kumekuja baada ya kukutana rais Felix Tshisekedi wa Kongo na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta mjini Luanda jana Jumatano katika wakati ambapo mivutano imeongezeka kati ya nchi hizo mbili majirani.

 Baada ya kikao hicho waziri wa mambo ya nje wa Angola akatoa tamko hilo la kufikiwa makubaliano ambayo pia yanaonesha pande hizo mbili zimeridhia juu ya kuondoka mara moja kwa waasi wa M23 kwenye maeneo wanayoyashikilia.

DR Kongo Flüchtlinge aus Flüchtlingslager Kanyaruchikya
Picha: Benjamin Kassembe/DW

Mkutano huu wa Luanda ulihudhuriwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye na aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye ni mpatanishi aliyeteuliwa na jumuiya ya Afrika Mashariki kusimamia juhudi za kurejesha amani na usalama Mashariki wa Kongo pamoja na rais wa Angola Juao Lourenco.

Rais Paul Kagame wa Rwanda hakuhudhuria mazungumzo hayo ingawa hakuna sababu zilizowekwa wazi mara moja kuhusu kutokuweko kwake huko Luanda.

Lakini pia mkutano huo wa Luanda haukulishirikisha kundi la waasi la M23,mnamo siku ya Jumanne serikali ya Kinshasa ilisisitiza kwamba haiwezi kukaa kwenye meza ya mazungumzo na waasi hao mpaka watakapoondoka kwenye maeneo wanayoyashikilia katika ardhi ya Kongo.

Na kimsingi waasi hao wamekamata sehemu kubwa ya mkoa wa Kivu Kaskazini na kuelekea mji mkuu wa eneo hilo,Goma.

DRC Goma Grenzzwischenfall
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano imeonesha kwamba washiriki wametaka mapigano yasitishwe kufikia kesho ijumaa magharibi na hatua hiyo itafuatiwa na waasi wa M23 kuondoka kwenye miji ya Bunagana,Rutshuru na Kiwanja.

Ikiwa M23 hawatofanya hivyo viongozi wakuu wa nchi watatowa maelekezo kwa vikosi vya kikanda kuchukua hatua za kuwalazimisha kuondoka.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW