1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Nagombea kuwa Rais wa Marekani yote

Hawa Bihoga
19 Julai 2024

Donald Trump amejitabiria ushindi mkubwa katika hotuba yake ya kukubali uteuzi wa kuwa mgombea urais wa chama cha Republican hapo jana, akiimarishwa machoni mwa wapiga kura na jaribio la kumuua.

https://p.dw.com/p/4iVQl
Milwaukee, Marekani | Donald Trump
Donald Trump akihutubia baada ya kukubali kuidhinishwa kupeperusha bendera ya Warepublikan.Picha: Mike Segar/REUTERS

Trump mwenye umri wa miaka 78 alisimama jukwaani kwa zaidi ya dakika 90, akisimulia kwa hisia namna alivyonusurika kifo kabla ya kugeukia malalamiko juu ya namna Wademocrat wanashughulikia uchumi, uhamiaji na masuala mengine.

Tutakuwa na hadithi ya ajabu, na tutaanza miaka minne mikubwa zaidi katika historia ya nchi yetu, alisema Trump kwenye Mkutano Mkuu wa chama cha Republikanmjini Milwaukee, ambapo alisisitiza kuwa anagombea kuwa rais wa Wamarekani wote.

"Nagombea kuwa Rais wa Marekani nzima, siyo Marekani nusu, kwa sababu hakuna ushindi kwa nusu ya Amerika. Alisema mwanasiasa huyo mkongwe

Aidha Trump aliongeta kwamba "usiku huu, kwa imani na kujitolea, nakubali uteuzi wenu kwa nafasi ya Rais wa Marekani."

Ilikuwa hotuba yake ya kwanza tangu kijana mwenye umri wa miaka 20 alipomfyatulia risasi na kusababisha jeraha kwenye mmoja ya maskio yake na kumuua mtu aliekuwa amesimama kando wakati wa mkutano wa hadhara mwishoni mwa wiki.

Soma pia:Trump aridhia kuwa mgombea urais wa Republican

Katika simulizi iliyojaa hisia juu ya tukio hilo la kupigwa risasi, ambapo Trump alisema Mungu alikuwa upande wake, rais huyo wa zamani aliomba muda wa kimya kumkumbuka mwathiriwa, askari wa zimamoto Corey Compatore, kabla ya kubusu kofia yake mbele ya umati uliokuwa unamsikiliza.

Lakini ingawa hotuba hiyo ilitajwa kuwa ni uzinduzi wa Trump asiye na hasira, anayetafuta umoja zaidi, alirejea mara moja kwenye kauli zake zilizozoeleka za kuichora Marekani kama taifa lililoharibiwa vibaya na linalohitaji kuokolewa.

Vipaumbele vya Trump alivyoahidi

Akiahidi kukamilisha ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, alisema uvamizi wa wahamiaji umeleta maangamizi na taabu kwa kile alichokiita taifa lililoporomoka. Aliahidi kukomesha matumizi makubwa ya Biden katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi aliyoyataka kuwa ni kashfa.

Donald Trump akihutubia mkutano wa Warepublikan
Donald Trump akihutubia mkutano wa WarepublikanPicha: Morry Gash/AP Photo/picture alliance

Trump alirudia pia madai ya uwongo kwamba Wademokrat walidanganya katika uchaguzi wa 2020 aliposhindwa na Biden, na licha ya wasaidi wake kuahidi kwamba Trump asingetaja hata jina la Biden katika hotuba yake, Trump alimtaja mpinzani wake na kile alichokiita uharibifu alioufanya.

Soma pia:Wapinzani wa Trump waungana kuonyesha mshikamano

Licha ya mkururo wa kashfa, mashtaka ya jaribio lake la kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020, na hatia 34 za uhalifu katika mashtaka ya mwezi Mei mjini New York, Trump anazidi kupanda juu katika kura za maoni ya wapigakura kuelekea uchaguzi mkuu wa Novemba.

Sherehe za kumuidhinisha Trump mjini Milwaukee zilikuwa kinyume kabisaa na mzozo unaomkumba Biden.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 81, alikaribia kulaazimishwa na chama chake kukaa pembeni na kutoa nafasi kwa makamu wake Kamala Harris au mgombea mwingine, huku wasiwasi ukiongezeka kwamba hali yake dhofu ya kiafya huenda ikasababisha kushindwa Novemba.

Mshauri mwandamizi wa Trump, Jason Miller, alisema hakuna kikubwa kitakachobadilika kwa Trump hata ikiwa Biden atajiondoa.